Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa
licha ya Tanzania kuendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya
ugonjwa wa Vikope (Trachoma) jamii bado inalojukumu la kuendelea
kuzingatia na kufuata kanuni za afya kwa kufanya usafi wa mwili na
mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Wadau wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dk.Neema Rusibamayila amesema kuwa Tanzania imepiga
hatua katika kupunguza ugonjwa huo ikishirikiana na wadau mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema
kupitia idadi ya wagonjwa wanaougua vikope imeendelea kupungua mwaka
hadi mwaka kupitia afua mbalimbali chini mpango ujulikanao kama “SAFE” ambao unahusisha huduma za Upasuaji,utoaji wa dawa za Antibayotiki, kuosha pamoja na usafi wa mazingira
Ameongeza
wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweza kufanikisha
upunguzaji wa ugonjwa huo kwa kutoa dawa/tiba kinga kwa wananchi katika
maeneo yaliyoathirika ambapo amesema kufuatia utafiti uliofanyika mpaka
sasa wilaya 22 ugonjwa huo umepungua sana kiasi cha wananchi wa maeneo
hayo kutohitaji dawa za tiba kinga.
Ameeleza
kuwa juhudi za sasa ni kuendelea kuwaelimisha wananchi kuendelea
kuchukua hatua kwa kufanya usafi ikiwemo unawaji wa uso pamoja pia
kuwaangalia wale waliokwisha kuugua ugonjwa wa Vikope (Trachoma) ili
waweze kufanyiwa upasuaji.
“Baada
ya mtu kupata ugonjwa huu kope za mgonjwa huingia ndani , kope za mtu
ambaye hana ugonjwa huu hutoka nje, zikiingia ndani zinakwaruza jicho na
mtu asipofanyiwa upasuaji kope zake mapema na kuziacha zikaendelea
kukwaruza jicho mwisho mgonjwa huyu hupata upofu” Amesisitiza
Rusibamayila.
Amefafanua
kuwa mashirika mbalimbali yamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha
zoezi hilo ikiwemo Shirika na la Msaada la Kimataifa la Uingereza (DFID)
pamoja na Mfuko wa Malkia ya Uingereza (The Queen Elizabeth Diamond
Jubilee Trust) ambao umekua ukitoa fedha kutokomeza ugonjwa wa Trakoma ,
shirika la Sightsavers, Shirika la Helen Keller International (HIK)
Tanzania pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ambayo mengine
yapo Kongwa mkoani Dodoma na Kilimanjaro ambao hushirikiana na wizara
kuwatafuta wagonjwa kwa lengo la kutoa matibabu.
Amesema
mpaka sasa kuna wilaya 18 ambazo zinakabiliwa na ugonjwa huo na
kufafanua kuwa juhudi za kuwapata walioathirika zinaendelea ikiwa ni
pamoja na kuwapata wale walioathirika kwa lengo la kuwafanyia upasuaji
na kuwapatia dawa ya tiba kinga pia kuwaelimisha ili waweze kubadili
tabia kwa kuwa wasafi.
“Tunaendelea
kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo uelimishaji wa wananchi wa maeneo
husika wachukue hatua, tunajua ugonjwa huu unaletwa na nzi, tunawahimiza
wananchi wanawe uso kuondoa uchafu na kuzuia nzi wanaosambaza ugonjwa
huo kutua kwenye macho yao” Amesisitiza Dk. Dk.Neema Rusibamayila.
Aidha,
amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuendelea kutambua mchango wa
Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo na pia kuendelea
kutimiza malengo ya kidunia ambayo yanaeleza kwamba ifikapo mwaka 2020
Tanzania iwe imeondoa ugonjwa wa vikope nchini.
Akizitaja
baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale
walioathirika katika maeneo yaliyo na ugonjwa huo hasa kwenye jamii za
wafugaji amesema ni pamoja na hali ya wananchi hao huishi
kwa kuhamahama pia sababu za mazingira hasa miundombinu ya barabara
ambayo imekua kikwazo cha kuzifikia jamii hizo hasa wakati wa kipindi
cha mvua.
Kwa
upande wake Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Upendo
John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa Tanzania
ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo zimekuwa zikinufaika na
fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Uingereza na DFID na mfuko wa
ulioanzishwa wa kumuenzi Malkia wa Uingereza kwa miaka 60 ya Utawala
wake unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Trakoma katika nchi
mbalimbali za Bara la Afrika Tanzania ikiwemo.
Amesema
ugonjwa wa Vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa Takwimu uko katika
wilaya 56 na kueleza kuwa kutokana na juhudi ambazo zimekuwa
zikichukuliwa na Serikali kuanzia mwaka 1990 hali inaonesha kuwa
maabukizi yameshuka hasa katika wilaya 22 ambako wananchi hawahitaji
tena ugawaji wa dawa.
Amesema
kuwa hali ya maambukizi katika maeneo hayo imekuwa zaidi kwa watoto na
wanawake kwenye maeneo yenye ukame na shida ya maji ikiwemo mkoa wa
Manyara na Dodoma na kubainisha kuwa mpaka sasa ni wilaya 18 ambazo
zinahitaji huduma ya dawa katika mkoa wa Arusha , Manyara, Dodoma katika
wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino.
“Naweza
kusema jitihada tunazofanya ni kubwa na kazi bado ipo hasa maeneo ya
wafugaji ambao baadhi yao wamekuwa wakitumia kifaa Fulani ambacho
kinaweza kunyofoa zile kope zinazowasumbua ili kuondoa usumbufu bila
kujua hali hiyo inatengeneza tatizo zaidi, ni changamoto kwetu,
tunahitaji kuendelea kuwaelimisha” Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa kupitia juhudi mbalimbali zilizofanyika wanajiandaa kufanya
tathmini katika wilaya zipatazo 10 katika kipindi cha mwaka huu
kuangalia maambukizi yamefikia wapi kwa lengo la kuongeza kasi ya
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma na kupunguza hali ya maabukizi
katika wilaya hizo.
Akizungumzia
idadi ya wagonjwa katika wilaya 56 ambazo maambukizi ya ugonjwa huo
yapo ilikadiliwa kwamba kuna maambukizi ya watu takribani 160,000 ambao
wameambukizwa tayari Vikope na kubainisha kwamba kuna mikakati
mbalimbali ilifanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
kuendesha upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo hali iliyoshusha kiwango hicho hadi kufikia wagonjwa 80,000 mwaka huu.
Amesema
chini ya ufadhili wa wadau hao wa miaka 5 wagonjwa takribani 50,000
wenye tatizo la vikope watafanyiwa upasuaji, huku Serikali kwa
kushirikiana na wadau wengine ikiendelea kutafuta fedha za kuwafikia
wagonjwa 30,000 watakaobaki.
Kwa
upande wake Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania
(DFID) Vel Gnanendra amesema kuwa wao kama wadau wa maendeleo
wataendelea kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha ugonjwa wa vikope
(Trachoma) unatokomezwa nchini.
“Tunafurahia
ushirikiano huu kutoa mchango wetu kuisaidia Tanzania kutokomeza
ugonjwa wa Vikope (Trachoma), kuzuia maumivu na mateso yanayosababishwa
na ugonjwa huu yanayowafanya watu kuangukia katika lindi la umasikini,
Tunaiahidi Serikali ya Tanzania kuwa kupitia ushirikiano huu
tutautokomeza ugonjwa huu na kubadili maisha ya wengi miaka ijayo”
Amesisitiza Gnanendra.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na
utokomezaji wa ugonjwa wa Vikope katika nchi mbalimbali za Bara la
Afrika ikiwemo Tanzania Dk. Aristid Bonifield amesema kuwa Mfuko huo
utaendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri katika
kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini.
Amesema
Mfuko wa Malkia Elizabeth utafanya kazi bega kwa bega na Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kuhakikisha kuwa hakuna mtanzania anayepoteza haki ya
kuonakutokana na ugonjwa wa vikope.
0 comments:
Post a Comment