TAMKO LA
MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO
NA MAZINGIRA) KUHUSU SHUGHULI ZINAZOTAKIWA KUFANYIWA TATHMINI YA ATHARI KWA
MAZINGIRA (ENVIRONMENTAL IMPACT ASSESSMENT)
TAREHE 2
JUNI, 2016
Ndugu Wananchi;
Katika ulimwengu wa sasa si rahisi
kutenganisha mazingira na maendeleo. Ni
wazi kuwa ufumbuzi wa matatizo ya uharibifu wa mazingira huwa mgumu kwa sababu
chanzo chake kimo katika mifumo ya uendeshaji wa shughuli za maendeleo ya
kiuchumi na kijamii yenye manufaa kwa uhai na ustawi wa binadamu. Shughuli
zinazosababisha uharibifu wa mazingira ndizo
hizo zinazomwezesha mwanadamu kuishi na kujiendeleza.
Hali ya mazingira inahusika sana na kuboresha
“mazingira” ya vitega uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi. Na kwa kweli, maliasili ya mazingira ndio msingi
wa maisha na maendeleo ya Watanzania.
Kwa mantiki hii, inabidi kutazama mambo mengi yanayochangia katika
uharibifu wa mazingira; kutambua matatizo ya mazingira katika undani wa
shughuli mbalimbali za maendeleo; kutambua sababu na kupima athari zake, na
kubuni mbinu au kuchukua tahadhari za kudhibiti au kuzuia uharibifu huo bila
kusimamisha wala kupunguza kasi ya shughuli za maendeleo.
Ni kwa sababu hii serikali imepitisha sera na
sheria za sekta mbalimbali zinazogusa mazingira na imebuni programu na miradi mingi ya
utekelezaji, katika kuhakikisha haya yanafanyika.
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu, Ofisi ya Makamu wa Rais
inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (SURA YA 191), pamoja
na Kanuni zake. Sheria hii ndiyo Sheria mama ya masuala yote yanayohusu
mazingira kwani Sheria hii inatekelezwa kwa kuzingatia sheria mbalimbali za
kisekta ikizingatiwa kwamba suala la mazingira ni suala mtambuka.
Sehemu ya Sita ya Sheria hii yenye kifungu cha 81 hadi cha 103
inaelekeza kila shughuli ya maendeleo ifanyiwe Tathimini ya Athari kwa Mazingira
na inatoa ufafanuzi wa hatua za kufuata.
Kifungu
cha 81(1) kimeweka wajibu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na
kubainisha katika Jedwali la Tatu la Sheria.
Ndugu
Wananchi;
Kimsingi mambo hayo yaliyotajwa katika Jedwali la Tatu la Sheria ni ya jumla. Melezo
ya kina yametolewa katika Kanuni za Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Ukaguzi
za mwaka 2005. Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi limebainisha orodha ya miradi ambayo inatakiwa kufanyiwa tathmini
kabla ya kuanza utekelezaji wake. Orodha hii imegawanyika katika makundi mawili
(2). Kundi la kwanza, yaani (A), ni la miradi ambayo lazima ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa
Mazingira kwani ni miradi ambayo inaonekana kuwa utekelezaji wake unaweza kuwa
na athari kubwa kwa mazingira, hivyo utafiti wa kina unahitajika ili kubaini
ukubwa wa athari na kupendekeza hatua mahsusi za kuepusha athari hizo.
Kundi la pili, yaani
(B), ni miradi ambayo inaonyesha kuwa utekelezaji wake unaweza kuwa na athari
kwa mazingira ingawa athari zake zinaweza kuwa ni ndogo ukilinganisha na miradi
iliyotajwa katika Kundi A. Miradi hii inatakiwa kufanyiwa Tathmini ya Awali ya
Mazingira (Preliminary Environmental Assessment) ili kuweza kuamua kama miradi
hii inaweza kuendelea bila kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (full
Environmental Impact Assessment). Hivyo kulingana na matokeo yatakayopatikana
katika Tathmini hiyo ya awali miradi iliyoko katika kundi hili inaweza
kuendelea bila kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira au kufanyiwa Tathmini
ya Athari kwa Mazingira.
Shughuli au miradi
inayohusika katika Kundi A, ambayo ni lazima ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa
Mazingira, ni kama ifuatavyo:-
·
Shughuli za kilimo: kilimo cha mashamba makubwa,
miradi ya kilimo inayohitaji kuhamisha makazi ya wanavijiji, uanzishwaji wa
matumizi ya mbegu mpya za mazao, uingizaji wa viumbe ambavyo vinasaba vyake
vimefanyiwa mabadiliko ya kijenetiki n.k;
·
Usimamizi wa mifugo na maeneo ya malisho: uswagaji
wa mifugo mingi, kuingizwa kwa spishi mpya au za kigeni;
·
Shughuli za misitu: ukataji wa mbao na utayarishaji,
ujenzi wa barabara ndani ya misitu ya hifadhi, biashara ya mkaa, kuni na
shughuli nyinginezo za uvunaji wa misitu, na kuanzisha biashara ya magogo au
kubadilisha matumizi ya ardhi ya misitu kwa matumizi mengine kwenye vyanzo vya
maji;
·
Shughuli za uvuvi: uvuvi wa kati na mkubwa, ufugaji
mkubwa wa samaki pamoja na ufugaji wa kamba, uzalishaji na hifadhi ya minofu ya
samaki viwandani;
·
Shughuli zinazohusiana na
wanyamapori: ukamataji wa wanyamapori na biashara ya
wanyamapori, kuanzishwa kwa maeneo ya uwindaji yanayohusisha uhamishaji wa
makazi ya vijiji, ranchi ya wanyamapori
na ufugaji na bustani na hifadhi za wanyapori;
·
Shughuli za utalii na burudani: ujenzi wa maeneo ya
kutembelea au hoteli pembezoni mwa fukwe za maziwa na bahari, kingo za mito na
visiwani; huduma za utalii na burudani katika maeneo yanayolindwa na maeneo
yanayozunguka (mbuga za wanyama, bustani za majini, hifadhi za misitu) kwenye
visiwa na maeneo yanayozunguka maji, ujenzi mkubwa kwa ajili ya michezo na
burudani;
·
Shughuli za madini: uzalishaji na usambazaji wa
umeme, gesi, utunzaji wa gesi asili, umeme wa maji, ujenzi wa miradi mikubwa ya
nishati jadidifu na isiyo jadidifu;
·
Bidhaa za petroli: Utafutaji na uchimbaji wa mafuta
na gesi, ujenzi wa mitambo ya kuzalisha mafuta na gesi, ujenzi au upanuzi wa
ghala la kuhifadhia petroli, gesi, diseli, lami ndani ya maeneo ya biashara,
viwanda na makazi ya watu, usafirishaji wa bidhaa za petroli;
·
Usafiri na mindombinu: ujenzi, upanuzi au
ukarabati wa barabara, viwanja vya ndege, reli na eneo la kutengeneza meli au
miundombinu ya bandari
·
Shughuli za chakula
na vinywaji: utengenezaji wa
mafuta yatokanayo na mimea na wanyama, machinjio, usindikaji wa tumbaku;
·
Viwanda vya nguo, ngozi, mbao, kemikali;
·
Shughuli za usafishaji na utupaji taka: ujenzi wa
mitambo ya uteketezaji taka, mtambo wa kuhudumia maji taka;
·
Shughuli za usambazaji maji: na
·
Shughuli za mipango ya maendeleo ya ardhi, nyumba na makazi: kuanzisha makazi mapya ya
watu na wanyama, miradi mikubwa ya mijini (ujenzi wa magorofa, vituo vya
magari, masoko n,k), ujazaji wa ardhi ikiwa ni pamoja na ardhi chini ya maji.
Aidha shughuli
zilizotajwa katika Kundi (B), ambazo ni lazima kufanyiwa Tathmini ya Awali ya
Mazingira (Preliminary Environmental Assessment) ni hizi zifutazo:-
·
Ufugaji wa samaki;
·
Ufugaji wa mifugo midogo wa mjini;
·
Ukulima wa mboga na maua;
·
Uzalishaji wa mkaa;
·
Utegaji wa ndege na biashara ya ndege pori;
·
Bustani za wanyama pori na ndege;
·
Kilimo cha mjini; na
·
Utengenezaji wa vigae.
Ndugu Wananchi;
Shughuli au miradi
iliyoelezwa hapo juu imetajwa kwa ufupi kwa kuwa ni vigumu kuandika vipengele
vyote vilivyotajwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 pamoja
na Kanuni zake kwa kuwa ni vingi mno. Hivyo, natoa wito kwa watu wote wanaotaka
kuwekeza katika shughuli yoyote kuitafuta, kuisoma na kuielewa Sheria hii
pamoja na Kanuni zake ili kuweza kuitekeleza kwa ukamilifu.
Ndugu
Wananchi;
Mtakumbuka tarehe 29 Mei, 2016 wakati nikitoa
Tamko kuhusu maadhimisho ya siku ya
Mazingira Duniani kwa mwaka huu nilieleza wazi kuwa Serikali imetoa miezi
miwili, hadi ifikapo tarehe 1 Agosti 2016 kwa wale wote ambao hawana Vyeti vya
Tathmini ya Athari kwa Mazingira katika shughuli zao waende Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira (Environmental
Audit).
Napenda kutoa wito kwa mara nyingine kwa wale
wote wanaofanya shughuli zilizoorodheshwa katika Kundi A na B katika Jedwali la
Tatu la Sheria ya Mazingira kuhakikisha kuwa wanatembelea Ofisi za NEMC mara
moja ili kuweza kupata utaratibu kamili wa kuwezesha shughuli zao kufanyiwa
Ukaguzi wa Mazingira. Niseme tu wazi kuwa baada ya muda uliotajwa hapo juu
kuisha hatutakuwa na uvumilivu kwa mtu yeyote ambaye atashindwa kutekeleza
agizo hili. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kuzifungia shughuli
hizo, kwa wale wote watakaoshindwa kutii na kutekeleza agizo hili. Hatutakubali
kisingizio cha kutoijua Sheria au kutojua mahitaji ya kufanyiwa Tathmini ya
Athari ya Mazingira.
Wakati huo huo, Serikali inapanga utaratibu wa
kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa
Mazingira ili upatikanaji wa vyeti hivyo usicheleweshe uwekezaji wa kibiashara
au shughuli za maendeleo.
January
Makamba (MB)
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano
na Mazingira
0 comments:
Post a Comment