Na Bashir Nkoromo
MWANASIASA
mkongwe nchini na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Agostine Mrema amewataka
wapinzani kumwacha Rais Dk. John Magufuli afanye kazi yake kwa kuwa
amechaguliwa kihalali na bado hajamaliza hata kipindi cha kwanza cha
uongozi wake.
Amewatahadharisha
wananchi kuwa makini na wanasiasa kwa kuwa wapo baadhi wasio na nia
njema na nchi badala yake wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi hata
kama nchi inaweza kuingia kwenye majanga.
Pia amevitaka
vyombo vinavyohusika na uratibu wa mambo ya siasa nchini hususan Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwatazama kwa macho mawili viongozi wa dini
wanaotumia nyumba za dini kuwa majukwaa ya kisiasa huku wakiwayumbisha
wananchi kwenye haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Aidha,
ametaja sababu iliyomfanya ashindwe kulichukua jimbo la Vunjo ambapo
pamoja na mambo mengine ni pamoja na hatua ya Rais Magufuli kumpigia
debe jimboni humo jambo lililowafanya wamwonee donge na kuhamishia
kampeni katika jimbo ili kuhakikisha halipati.
Hayo
aliyasemwa jana mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, alipokuwa
akizungumzia hali ya kisiasa ya hapa nchini, ambapo alisema analaani
kitendo cha wapinzani kudai Rais Magufuli hawatendei haki wananchi,
anavunja sheria, katiba na anakiuka haki za binadamu na kuua demokrasia
ya nchi.
Mrema alisema
hivi sasa nchini kumeibuka vuguvugu la kisiasa hususan kwa wapinzani
kutangaza serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. Magufuli imekuwa
ikikiuka haki za binadamu na kuponda demokrasia jambo ambalo si la kweli
kwa kuwa kila mwanasiasa yupo huru kuzungumza na kuchangia maendeleo
kwa kadri anavyoweza.
Alisema wapo
wanasiasa wanaodai Rais Magufuli hawatendei haki wananchi, anavunja
sheria na kukiuka haki za binadamu huku wasemao hayo ndio vinara wakuu
wa kukiuka haki hizo.
"Wapinzani
wenzangu ndio vinara na waliokubuhu na vitendo vya kuaribu demokrasia
nchini na kuwapotosha wananchi jinsi ya katiba inavyoenda
nchini,"alisema Mrema.
Aliongeza
kuwa kipindi cha uchaguzi mwaka jana, Mbunge wa Vunjo James Mbatia
alikiuka sheria na maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani wa
mwaka 2015.
Mrema ambaye
pia amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo, alisema NEC na taasisi zingine
zinazosimamia shughuli za kisiasa nchini zinapaswa kuwa makini na baadhi
ya viongozi wa dini ambao wameacha jukumu lao kuu la kuwajenga kiroho
waumini wao na kutumia vyombo vya dini kama kinga yao kwenye siasa.
"Wakati wa
harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka jana wapo viongozi wa dini
waliosimama kwenye nyumba za ibada na kuwahubiria wafuasi wao kwamba
mwaka huu rais lazima atoke kanda ya Kaskazini na nje ya hapo hatuwezi
kukubali. Maneno hayo hayapaswi kuachwa yaendelee kwa kuwa ni hatari kwa
mustakabbali wa siasa na maendeleo ya demokrasi hapa nchini.
"Wananchi
kuweni makini si kila mwanasiasa anayekuja mbele yenu ana nia njema na
taifa hili wengine lengo lao ni kutaka nchi iingie kwenye matatizo ili
wao wanufaike,"alisema.
Akizungumzia
kwa nini alikosa ubunge wa vunjo kupitia uchaguzi huo, alisema hilo
lilitokana na mkakati wa wapinzani wenzake ambao walimuonea donge baada
ya kuungwa mkono na Rais Magufuli aliposimama jimboni humo wakati wa
kampeni na kumnadi.
"Nawashangaa
wapinzani wenzangu hawajui kuwa Rais Dk. Magufuli anathamini zaidi
mchango wangu nilioutoa nilipokuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri Mambo ya
Ndani ya Nchi, jinsi nilivyokuwa nafanya kazi kwa nguvu moja kwa ajili
ya kuliletea taifa maendeleo,"alisema.
Aidha, Mrema
alisema ana uhakika endapo Dk. Magufuli atakabidhiwa uenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), atamtafutia nafasi ya kumsaidia kushughulika na
maendeleo ya Tanzania kwa kuwa kasi yake anaimudu na ataweza kwenda nae
sawa.
Hivi karibuni
vyma vya upinzani hususan vinavyounda UKAWA vbimekuwa na kampeni ya
kutaka kuzunguuka nchi nzima kuishitaki serikali kwa madai imekuwa
ikikandamiza haki hapa nchini.
Hata hivyo,
tayari polisi imepiga marufuku mikutano, makongamano na maandamano
yoyote ya kisiasa kwa kuwa yanamwelekeo wa kuwachochea wananchi kukiuka
sheria za nchi na kushiriki matukio ya uvunjifu wa amani.
0 comments:
Post a Comment