Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiwahutubia Wanachama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) mara alipowatembelea katika eneo lao la kazi, 28 Juni, 2016. |
Na Benedict Liwenga
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameahidi kuzitataua baadhi ya changamoto mbalimbali
zinazoikabili Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) ikiwemo
upatikanaji wa Hati Miliki ya Kiwanja kwa ajili ya kazi zao, Ushuru unaotozwa
kupitia Idara ya Maliasili nchini pamoja na Sheria ya Tozo katika Viwanja vya
Ndege.
Mhe, Nnuaye ametoa ahadi hiyo leo
jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Wanachama wa Shirikisho hilo ambapo
amesema kuwa, suala la upatikanaji wa Hati Miliki ya eneo kwa ajili ya kazi za
Wachongaji hao alishaanza kuifanyia kazi kwa kufanya mawasiliano na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na amewahakikishia
kwamba Hati ya eneo hilo itapatikana ili Wachongaji hao waweze kuwa na eneo lao
maalum la kazi zao.
''Suala la upatikanaji wa Hati
Miliki katika eneo lenu ambalo limekuwa likileta minong’ono niachieni mimi
kwani najua katika hili kuna baadhi ya watu wenye fedha wanataka kuwakandamiza
watu wasio na uwezo kwa kudai kuwa eneo ni la kwao, hapo awali nilishafanya
mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na
nawahahakikishieni kuwa haki itatendeka, kwani hakuna mtu mwenye mfuko mkubwa
wa kuweza kuiingiza Serikali nzima katika suala hili’’, alisema, Mhe. Nnauye.
Kuhusu suala la Ushuru unaotozwa na
Maliasili nchini, Mhe. Nnauye amesema kuwa yuko tayari kukaa na watu wa
Maliasili na kuona namna gani ushuru huo unavyotozwa hususani kwa Wachonagji
hao pasipo kuonewa mtu ambapo pia ameshauri kuwa baadhi ya kodi ambazo
zinazoweza kuua biashara za watu wenye vipato vya chini ni vema zikaondolewa
ili zisiendelee kuwaumiza.
Aidha, Mhe, Nnauye ameahidi
kutembelea maeneo ya Viwanja vya ndege ili kuweza kujua baadhi ya bidhaa za
kazi za Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa na Watendaji viwanjani hapo
zimekuwa zikiishia wapi ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa katika viwanja
hivyo.
‘’Niwahakikishieni kwamba nitakwenda
mwenyewe katika viwanja vya ndege ili nijue ukweli wa malalamiko yenu kwamba
kumekuwa na baadhi ya kazi zenu za sanaa kama vile Uchongaji ambazo zimekuwa
zikikamatwa katika baadhi ya viwanja vyetu vya ndege lakini mwisho wa siku
hazijulikani zinaishia wapi’’, Alisema, Mhe. Nnauye.
Mhe. Nnauye ameahidi pia kujenga
utaratibu wa kutembelea maeneo ya kazi za sanaa mara kwa mara na kwa namna
nyingine amewaasa Kampuni ya Quality Group kusaidia kuzitangaza kazi za sanaa
za Wachongaji hao kwani wao wameshafungua Duka Maalum ambalo linarahisisha
upatikanaji wa bidhaa za sanaa kwa wageni na wenyeji ili kuwasaidia Wachongaji
hao nchini.
Sambamba na hayo, Mhe. Nnauye
amewashauri Wanachama hao kuunda SACCOS imara ambayo itawasaidia katika
kujikwamua kiuchumi kutokana na kazi zao na kuwaahidi kuwatafutia mitaji kwa
makubaliano ya kwamba, wanapaswa kuwachagua viongozi waaminifu ambao wanaweza
kuongoza vema Saccos hiyo kwa manufaa ya wanachama wote.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha
Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA), Bw. Adrian Nyangamalle amepongeza
juhudi za Serikali katika kuwasimamia Wasanii kote nchini ambapo ameiomba
Serikali pia kuharakisha suala la upatikanaji wa Sera ya Sanaa pamoja na Mfuko
wa Sanaa kwa ajili ya Wasanii hao.
‘’Nikuombe Mhe. Waziri kutusaidia
kuzishawishi baadhi ya Taasisi na Makampuni nchini kujenga utarataibu wa
kuwatembeza wageni wanaokuja nchini katika maeneo ya sanaa ili soko la bidhaa
zetu liweze kukukua ndani na nje ya nchi yetu’’, alisema Bw. Nyangamalle.
Chama cha Wasanii na Wachongaji
Tanzania (CHAWASAWATA) kilianzishwa mnamo mwaka 1984 na kimesajiliwa kihalali
na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ambapo mbali na majukumu yake kimeweza
kuwaandaa na kuwashirikisha Wasanii wa ndani na nje ya nchi pamoja na kutetea
Wasanii katika kupata haki zao.
0 comments:
Post a Comment