NAO WANUNUZI WANAENDELEA KUPATA HUDUMA HII YA WAMACHINGA KATIKA MAENEO YA UHINDINI JIJINI MBEYA.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
-JIJI LA KIRI WAMACHINGA KUTOVAMIA MAENEO.
-WAPO KWA MUDA WAKATI SERIKALI IKIKAMILISHA MAENEO
WALIYOTENGEWA.
-WAMACHINGA WASEMA TUPO TAYARI KUHAMIA MAENEO
MAPYA
HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, imesema
wafanyabiashara ndogondogo maharufu kwa jina la (Wamachinga) hawajavamia maeneo
wanayofanyia biashara zao sasa bali wapo kwa muda wakati serikali
ikikamilisha miundombinu kwenye maeneo waliyoyapendekeza.
Wamachinga hao ni wale wanaoendeshea biashara zao
kandokando ya barabara inayoingia kwenye soko kuu la Mwanjelwa pamoja na wale
wa barabara inayoanzia eneo la Mafiat kuelekea Soko Matola.
Awali, halmashauri ya Jiji la Mbeya, iliwaondoa wa
machinga bila ya kuwashirikisha jambo lililopelekea wafanyabiashara
hao kufanya vurugu zilizoambatana na
kufunga barabara katika eneo la Mwanjelwa, wakipinga kuondolewa
katika eneo wanalofanyia biashara zao ndogondogo bila kuoneshwa eneo jipya.
Akizungumza na Freedonia Leo kwa njia ya
simu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Juma Iddy alikiri kuwepo kwa
wamachinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na kwamba wapo kwa muda wakati
wakisubili kukamilishwa kwa eneo maalumu walilotengewa.
“Wamachinga hawajarudi, wapo kwa muda
wakati serikali ikikamilisha baadhi ya miundombinu kwenye maeneo mapya na ifikapo
Mei 30 mwaka huu maeneo hayo yatakuwa yamekamilika,” alisema
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni eneo la
barabara ya Bulongwa-iliyopo nyuma ya Soko jipya Mwanjelwa, eneo la Chuo cha
wafanyakazi(OTTU) pamoja na eneo Moondust-Soweto.
Aidha, Iddy alifafanua kuwa ifikapo Juni
15, mwaka huu wamachinga hao watatakiwa kuhamia kwenye maeneo hayo na endapo
watakaidi agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Wamachinga kwa upande wao walisema, wapo
tayari kuondoka kwenye barabara hizo endapo serikali itawapeleka kwenye maeneo
ambayo wameyapendekeza.
“Tupo tayari kuondoka kwenye eneo hili la
barabara kama serikali itafuata mapendekezo yetu kuhusu eneo
tunalolihitaji,”alisema John Kadege
Alisema, moja ya eneo walilolipendekeza ni
kandokando ya Benki ya Posta mbali na lile walilopatiwa wahanga wa moto wa soko
kuu la Uhindini.
Freedonia Leo, lilifanikiwa kuzungumza na
mmoja wa wanunuzi wa bidhaa hizo zilizotandazwa kandokando ya barabara Alex
Sichale, alisema kitendo cha wafanyabiashara hao kuendesha biashara kandokando
ya barabara ni ukiukwaji wa sheria pia ni usumbufu kwa wapita njia pamoja na
waendesha magari.
Akizungumzia suala hilo Diwani wa Kata ya
Forest Boyd Mwabulanga kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
alisema wamachinga wanatakiwa kutii na kutekeleza sheria mbalimbali ikiwemo ya
uendeshaji wa biashara katika maeneo maalumu.
“Halmashauri ipo katika hatua za mwisho
za ukarabati wa miundombinu katika maeneo yaliyopendekezwa na wamachinga
wenyewe hivyo watakapotakiwa kuondoka basi kusiwepo na siasa,”alisema
Freedonia Leo, lilifanikiwa kuzungumza na
Diwani wa Kata ya Itezi Frank Mahemba kupitia chama cha
mapinduzi(CCM) ambaye alisema mzungumzaji wa suala hilo ni Meya wa Jiji la
Mbeya.
Jitihada za kumpata Mstahiki Meya wa Jiji
la Mbeya Athanas Kapunga zilishindikana baada ya kumkosa ofisini na
alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment