JESHI la Polisi mkoani Mbeya limeanzisha
kituo kidogo cha Polisi katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe ili
kuimarisha ulinzi kwa abiria na wageni mbalimbali wanaosafiri.
Akithibitisha kuanzishwa kwa
Kituo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Songwe unapokea wageni mbalimbali kutoka ndani na Nje ya
Nchi hivyo unahitajika ulinzi ili wageni wawe katika hali ya usalama.
Alisema mbali na kuimarisha
ulinzi kwa kuanzisha kituo kidogo cha Polisi pia anajipanga kuhakikisha kinakua
na vitendea kazi vyote muhimu ikiwemo kuwepo wa Askari wa kutosha.
Aliongeza kuwa analazimika
kuongeza ulinzi kutokana na tukio la hivi karibuni ambalo watu wasio waaminifu
walivunja na kuiba Televisheni moja ya ukutani pamoja na kamera ya ulinzi
katika mgahawa uliopo ndani ya uwanja huo.
Hata hivyo alisema wezi hao
walishakamatwa na upelelezi unaendelea ili waweze kufikishwa mahakamani kwa
ajili ya kesi inayowakabili kwani picha zao zilionekana katika Kamera zingine
ambazo hawakuziona.
Aidha alitoa wito kwa wananchi
wa Mkoa wa Mbeya wanaoishi na kufanya shughuli zao kuuzunguka uwanja wa ndege
wa Kimataifa wa Songwe kuwa sehemu ya ulinzi wa Uwanja huo kwa kutoa taarifa
pindi wanapobaini kuwepo kwa dalili za uhalifu.
Naye Meneja wa Uwanja wa Ndege
Songwe, Hamis Amir alisema kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa kituo cha Polisi
Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kukarabati moja ya majengo yaliyopo uwanjani
hapo kwa ajili ya matumizi ya kituo cha Polisi.
Alisema awali walikuwa
wakitumia makampuni binafsi ya ulinzi ambayo uongozi wa Uwanja uliingia nao
mkataba huku Jeshi la Polisi likifanya doria nyakati za usiku pekee tena kwa
muda mfupi.
Alisema uwepo wa kituo cha
Polisi kutasaidia kuimarisha ulinzi wa mali za Uwanja pamoja na usalama wa
abiria katika kipindi ambacho Serikali inatarajia kumalisha ufungaji za Taa za
kuwezesha ndege kutua nyakati za usiku na kiangazi sambamba na kukamilika kwa jingo
la abirialenye uwezo wa kubeba abiria 450 kwa wakati mmoja.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment