Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ameviagiza vyombo
vinavyohusika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Williamson
Diamond Ltd na wote waliohusika kuidhinisha usafirishaji wa madini ya
almasi kutoka migodi ya kampuni hiyo na kudanganya thamani halisi ya
madini hayo kwa lengo la kuisababishia hasara Serikali.
Dkt.
Mpango ametoa agizo hilo leo tarehe 09 Septemba, 2017 baada ya kukagua
madini ya almasi yaliyokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam yakisafirishwa kupelekwa nchini
Ubelgiji.
Miongoni
mwa hatua za kisheria ni pamoja na kutaifisha madini yote ya almasi
yaliyokamatwa baada ya kubainika udanganyifu wa thamani yake halisi,
kuwakamata na kuwachunguza wote waliohusika katika udanganyifu huo
wakiwemo wajumbe wa bodi zilizomaliza muda wake na wafanyakazi waliopo
na waliostaafu.
Almasi
hiyo ilikamatwa tarehe 31 Agosti, 2017 muda mfupi kabla ya kupakizwa
kwenye ndege ili isafirishwe kwenda nchini Ubelgiji, na ilipochunguzwa
ilibainika kuwa nyaraka za kampuni ya Williamson Diamond Ltd zimeonesha
kuwa almasi hiyo ina thamani ya Dola za Marekani Milioni 14.798 sawa na
Shilingi Bilioni 33 za Tanzania wakati thamani yake halisi ni Dola za
Marekani Milioni 29.5 sawa na Shilingi Bilioni 65 za Tanzania.
Kabla
ya kukagua almasi hiyo Waziri Mpango amepokea taarifa ya timu ya
wataalamu iliyofanya tathmini ya thamani halisi ya madini hayo ambapo
kiongozi wa timu hiyo Prof. Abdulkarim Mruma amesema pamoja na kubaini
upotevu mkubwa wa fedha, kuna dosari nyingine zikiwemo kukosekana kwa
vifaa ya kupimia madini hayo, almasi kusafirishwa na kuuzwa sokoni bila
uwepo wa mwakilishi wa Serikali na ameshauri hatua za udhibiti huo
zifanyike katika madini yote yanayochimbwa hapa nchini.
Pamoja
na kuipongeza timu iliyofanya tathmini hiyo na vyombo vya dola
vilivyokamata madini hayo Waziri Mpango amesema Serikali itatekeleza
ushauri wote uliotolewa na timu ya Prof. Mruma na kwamba kuanzia sasa
almasi inayozalishwa hapa nchini itasindikizwa na maafisa wa Serikali
hadi sokoni na inataka kuanza kupokea gawio halali kutoka mgodi huo.
Waziri
Mpango ametoa maagizo hayo mbele ya viongozi wa vyombo mbalimbli
wakiwemo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles
Kichere, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Biswalo Mganga, Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Brigedia Jenerali John Julius Mbungo, Kamishna wa Madini Tanzania
Mhandisi Benjamin Mchwampaka na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam
SACP – Lazaro Mambosasa.
0 comments:
Post a Comment