Na Moses Ng’wat, Rungwe.
MADIWANI wa Halmashauri ya Rungwe
wamesusia posho ya kikao cha kupitia na kujibu hoja za
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu (CAG ) kwa madai kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Loema Peter,
amezipunguza bila kuwafahamisha.
Madiwani hao 38 wamegomea posho
ya shilingi 100000 wakitaka kulipwa posho ya
awali shilingi 150,000, huku wakilalamikia kutolipwa
malimbikizo ya posho ya mwezi ambayo hawajalipwa kwa miezi
minne.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada
ya kikao hicho kilichosimamiwa na Mkuu wa Mkoa, Amos
Makalla, kumalizika ambapo madiwani hali walikataa kusaini
kiasi hicho wakidai ni pungufu tofauti na walivyokuwa
wakilipwa awali.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ezekiel
Mwakota, alikiri kususia posho hiyo , huku akisisitiza ni
haki ya Madiwani kwa kuwa hawakupewa taarifa kama kuna
mabadiliko katika utaratibu mpya wa malipo ya posho za
Madiwani.
“Suala hilo linajadiliwa kwenye
vikao, ni haki yao Madiwani kutochukua kiasi hicho cha fedha
kwani hawakuwa na taarifa yeyote ya mabadiliko, lakini
ukweli ni kwamba kuna mabadiliko posho za Madiwani
wanahitaji ufafanuzi”.
Mwakota aliongeza kuwa, Madiwani
wanalipwa posho ya mwezi kutokana na makusanyo ya mapato ya
ndani, hivyo kwa kipindi cha miezi mitatu wameshindwa
kulipwa kutokana na kusuasua kwa ukusanyaji.
“Ni kawaida jambo hili hapa Rungwe ni
la muda mrefu na ni kama utaratibu tuliojiwekea kuwa,
Madiwani wawe wa mwisho kulipwa…huwezi kulipa Madiwani
kwanza wakati kuna watendaji wengi hawajalipwa”.
Aliongeza kuwa suala hilo linaendelea
kujadiliwa na Madiwani hao watalipwa madai yao yote ndani ya
muda mfupi, hasa kwa fedha za mwezi Mei na Juni kwa kuwa
mchakato wa fedha hizo tayari umefikia hatua nzuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
hiyo, Loema alipoulizwa juu ya tukio hilo hakuwa tayari
kulizungumzia na kusema suala hilo halijafika kwake.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment