Pages

Ads 468x60px

Thursday, January 17, 2013

SERIKALI YATAKIWA KUONDOA UKIRITIMBA KWENYE BIASHARA YA MAFUTA YA NDEGE


WAKATI ndoto ya adha ya usafiri wa anga ikikamilika kwa mara ya kwanza mkoani Mbeya, serikali imetakiwa  kuondoa ukiritimba katika biashara ya mafuta ya ndege hapa nchini.
Hali hiyo inadaiwa kuwa imekuwa ikiyabebesha mzigo mkubwa  makampuni yanayotoa huduma hiyo, abiria pamoja na kudumaza biashara ya usafirishaji wa anga hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana, Jijini hapa na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, washirika la ndege binafsi hapa nchini la Precsion, Michael Shirima, katika tafrija ya uzinduzi wa safari za anga katika mkoa wa Mbeya iliofanya na shirika hilo.

Alisema kuwa moja ya changamoto inayokwaza sekta ya usafirishaji wa anga nchini, ni serikali kuendelea kuruhusu sheria ya ukirimba ya ambayo imekuwa na masharti magumu ya watu binafsi kuwekeza katika biashara ya mafuta ya ndege kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini.
Kukosekana kwa  visima vya mafuta ya ndege katika viwanja vingi tunavyovitumia ni changamoto kubwa kwa kuwa tunalazimika kupunguza idadi ya abiria kwa lengo la kubeba kiasi kikubwa cha mafuta, hivyo tunaomba serikali iondoe ukiritimba huu ”.
Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesababisha kupunguza ufanisi wa makampuni kwa kuwa mengi hulazimika kupunguza idadi ya abiria kutoka 70 hadi kufikia 50 ili nafasi ya abiria waliopungua itumike kubeba shehena ya mafuta .

Akizungumzia hatua ya kampuni hiyo kuanzisha safari mkoani hapa, Shirima alisema hali hiyo imetokana na utafiti wa kina uliofanywa na kampuni hiyo na kubaini kuwepo kwa mahitaji makubwa ya huduma ya usafiri wa anga kwa wananchi wa mikoa ya nyanda za juu kusini na nchi za kusini mwa afrika.

Aliongeza kuwa licha ya Mkoa wa Mbeya kukosa huduma za uhakika za usafiri wa anga kwa zaidi ya miaka 40, anaamini kuwa ni eneo zuri kwa biashara hiyo na fursa adhimu ya kufunguka kwa milango ya maendeleo yatakayokuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Awali akimkaribisha Mkurugenzi huyo wa bodi, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, aliwataka wananchi, wafanyabiashara na makampuni makubwa mkoani hapa kutumia fursa ya ujio wa shirika hilo kusisimua biashara zao.

Hata hivyo alisema tatizo kubwa linalochangia umasikini wa waafrika ni kushindwa kutumia vizuri rasilimali muda, hali ambayo imeendelea kuzorotesha mipango mingi ya maendeleo.
Hebu tujiulize, kama unapoteza fedha muda huu baadae unaweza kuzipata, lakini ukipoteza muda hivi sasa siamini kama unaweza kuupata tena, hivyo ni vizuri tukatumia vizuri muda wetu ili kukimbizana na maendeleo.” Alisema Sigalla.

0 comments:

Post a Comment