INAPOFIKA saa tisa alasiri, siku kama ya leo, maarufu kama Ijumaa Kuu, katika nyumba za ibada za Kikristo, kimya hutanda, mishumaa huzimwa na kuashiria kuwa ni siku ya majonzi.
Ijumaa
Kuu ni siku ambayo Wakristo duniani kote hukumbuka mateso aliyoyapata Yesu
baada ya kusulubishwa msalabani yapata zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeipa thamani siku hii kwa kuitangaza
kuwa ya mapunziko.
Siku
hii huadhimishwa kwa ibada inayoambatana na kusoma mistari ya Biblia
inayoelezea undani wa matukio yaliyosababisha kusulubiwa kwa Yesu Kristo.
Hii
ni siku ambayo inatajwa kuwa na maana kubwa katika imani ya Kikristo. Waumini
wanaamini kwamba, kusulubiwa na kufa kwa Yesu, kumeleta ukombozi duniani kote.
Ijumaa Kuu haithibitishwi tu na vitabu vya dini, bali hata machapisho ya
kihistoria, yanathibitisha juu ya kusulubiwa na kufa kwa Yesu.
Huadhimishwa
kwa ibada huku zikitawaliwa na mistari na nyimbo za maombolezo ya kufa kwa
Yesu. Rangi za vitambaa vipambwavyo kanisani, huwa ni zile zinazoashiria maombolezo.
Hufanyika tangu asubuhi na inapofika saa tisa, muda unaosadikiwa kuwa ndipo
Yesu alikata roho, makanisa hutawaliwa na kimya kiambatanacho na kuzima
mishumaa ndani ya kanisa. Katika muda huo wengi hutafakari namna
walivyokombolewa kwa damu ya Yesu.
Makanisa
mengi, vikundi mbalimbali kama vile watoto, vijana na wanawake, hutumia siku
hiyo kuonesha maigizo ya kusulubiwa na kufa kwake. Majina yanayotumika katika
mataifa mbalimbali, yote hushabihiana kwa kuonesha nafasi ya siku hii. Ingawa
majina hayo huweza kutofautiana kulingana na lugha itumikayo katika eneo
fulani, lakini yote hulenga kuzungumzia nafasi na umuhimu wa Ijumaa Kuu.
Katika
lugha ya Kijerumani, siku hii hujulikana kwa jina la Karfreitag linalomaanisha
kuwa ni Ijumaa ya Maombolezo. Waisrael wanaiita Big Friday wakimaanisha ni siku
kubwa na maalumu. Nchi za Amerika ya Kilatini, Spain, France, Italia, Ufilipino
na Ureno wanaiita Ijumaa Takatifu. ‘Sexta-Feira Santa’ ni neno la Kireno lenye
kumaanisha Ijumaa Takatifu.
Katika
nchi zenye Wakristo wengi, kama vile Ujerumani, Uingereza Canada na New
Zealand, hii ni siku ya mapumziko. Nchi nyingi zinazozungumza Kingereza, maduka
mengi mitaani hufungwa kwa ajili ya kuadhimisha siku hii. Nchini Canada, benki,
ofisi za serikali na shughuli zote za watu binafsi hufungwa siku hiyo.
Katika
Jamhuri ya Ireland, ambayo ni nchi ya Kikatoliki, pombe huzuiwa kuuzwa wakati
wa Ijumaa Kuu. Karibu sehemu za starehe na migahawa mingi nchini humo hufungwa
kwa siku nzima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo kuu. Nchini
Ujerumani, ni makosa kufanya maonesho na shughuli mbalimbali za starehe kama
vile kucheza muziki siku ya Ijumaa Kuu.
Hatua
hiyo ambayo huwagusa hata wasio Wakristo, katika mwongo uliopita, iliwahi kuzua
upinzani. Nchini Afrika Kusini, Sheria inatamka kufunga ofisi zote za serikali,
shule wakati wa Ijumaa Kuu. Baadhi ya maduka hufungwa pia. Kuuza au kununua
pombe pia kunakatazwa. Hapa nchini pia siku hii imo katika orodha ya siku
zinazotambulika kuwa ni za mapumziko.
Mafundisho
yanasema kwamba sambamba na waumini kuhudhuria ibada, Ijumaa Kuu ni siku kuu
ambayo haina budi kutumiwa na Wakristo kutubu dhambi. Ni siku inayowakumbusha
upendo wa dhati aliouonesha Kristo. Haipaswi kuchukuliwa kuwa siku ya mapumziko
marefu pekee bali na wao pia kutafakari namna wanavyoonesha upendo kwa wengine
na kuzidisha kufanya mambo yanayompendeza Mungu.
Ziko
tamaduni mbalimbali walizojiwekea Wakristo wengi wakati wa Siku ya Ijumaa Kuu.
Miongoni mwake, ni ulaji au kutokula aina fulani ya vyakula na kufunga kula.
Hata hivyo, Wakristo wengi hawasubiri kufunga wakati wa Kwaresma au Ijumaa Kuu
pekee, bali hufanya hivyo siku zote.
Viongozi
wa dini wanafundisha kwamba kujinyima ni jambo la msingi na hivyo inatakiwa iwe
ni kujinyima kitu fulani lakini wakati huo huo hicho ulichojinyima kitumike
kumsaidia mwenye shida. Licha ya baadhi ya watu kufunga siku ya Ijumaa Kuu wapo
ambao wamejiwekea utaratibu wa kufunga kila Ijumaa wakati wengine hufunga siku
40 kabla ya Pasaka.
Suala
la kufunga linaloambatana na kutenda yaliyo mema, halina muda wala kikomo.
Ulaji wa mkate mdogo aina ya keki hususan kwa jamii za Waingereza, pia ni
utamaduni mwingine uambatanao na maadhimisho ya Ijumaa Kuu. Vile vile nyama, ni
chakula ambacho waumini wengi wa Kikristo huiepuka.
Wakati
awali ilizoeleka kwamba waumini wa madhehebu ya Katoliki ndio wenye utamaduni
huo, lakini uchunguzi unonesha kwamba wapo waumini katika madhehebu mengine
wanaozingatia pia utamaduni huo. Baadhi ya Walutheri katika nchi za Sweden,
Scandinavia, Ujerumani na hata hapa nchini pia wanazingatia utamaduni wa
kutokula nyama wakati wa Ijumaa Kuu.
Baadhi
ya viongozi wa dini husema kwamba suala la kutokula nyama Ijumaa Kuu siyo
imani, bali ni utamaduni. Yaani huchukuliwa kama jukumu binafsi
lisilomlazimisha mtu. Viongozi wa dini wamekuwa wakifundisha kwamba maadhimisho
ya Pasaka yanapaswa kuambatana na tafakuri kuhusu njia bora za kuendeleza amani
kwa mtu binafsi na hata nchi kwa ujumla.
Katika
kipindi hiki ambacho nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya kuimarisha
amani na upendo, kwa mfano, Pasaka inaweza kutumika katika kurejesha hali ya
kuvumiliana ili kuepuka migogoro ya kisiasa na kijamii.
0 comments:
Post a Comment