MBEYA PRESS CLUB
TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA LA
KULAANI KUPIGWA KWA MWANDISHI WA HABARI RASHID MKWINDA WAKATI WA MECHI YA MPIRA
WA MIGUU BAINA YA KIMONDO FC NA NJOMBE FC ILIYOFANYIKA JUNI 2 KATIKA UWANJA WA
KUMBUKUMBU YA SOKOINE JIJINI MBEYA.
RASHIDI MKWINDA MWANDISHI WA HABARI ALIYEPIGWA NA TIM YA NJOMBE MJI
JUNI 2, mwaka huu kulikuwa na mechi
ya mpira wa miguu ya Ligi ya Mabingwa wa mikoa baina ya timu ya Kimondo FC ya
Mbozi mkoani Mbeya na Njombe FC ya Mkoa mpya wa Njombe, mchezo uliofanyika
katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.
Wakati mchezo huo ukiendelea,
wandishi wa habari kama ilivyo kawaida yao walifika uwanjani hapo kutekeleza
wajibu wao wa kuchukua habari na kuuhabarisha umma wa watanzania.
Wakati wa mapumziko ulipofika,
wachezaji wa Timu ya Kimondo FC waliingia kwenye chumba chao cha kubadilishia
nguo, lakini wachezaji wa timu ya Njombe FC hawakwenda kwenye chumba chao cha
kubadilishia nguo na badala yake walibakia uwanjani na kwenda kukaa mahali
lilipokuwa benchi la ufundi la timu hiyo.
Mwandishi wa Habari wa Gazeti la
Majira Rashid Mkwinda ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Wandishi wa Habari
Mkoa wa Mbeya alikwenda kuwapiga picha wachezaji hao ambao kwa wakati huo
walikuwa pamoja na viongozi wa timu hiyo.
Kitendo hicho kilisababisha golikipa
wa timu ya Njombe FC, Joshua Mwampegeje kuanza kumtolea matusi mwandishi huyo,
huku wachezaji wengine pamoja na viongozi wao wakimfuata na kuanza kumpiga,
kumjeruhi, kusababishia uvimbe na maumivu mwilini na kumvunjia kamera yake
wakati akitimiza wajibu wake.
Mashabiki wa Njombe FC waliokuwa
Jukwaani walipoona vurugu hizo nao waliingia uwanjani na kushirikiana na
viongozi na wachezaji wa timu yao kumpiga mwandishi na kumjeruhi.
Tukio hilo lilikuwa likishuhudiwa na
viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) ambao walikuwa
wamekaa kwenye jukwaa kuu wakishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea
uwanjani hapo bila ya kuchukua hatua yoyote.
Aidha wachezaji hao walifanikiwa
kumpiga, kumjeruhi na kumvunjia kamera mwandishi huyo kutokana na kutokuwepo
kwa ulinzi wa aina yoyote uwanjani hapo, hali ambayo pia ilisababisha mashabiki
kuingia kirahisi uwanjani na kuongeza ukubwa wa vurugu.
Kutokana na kitendo hicho, Chama cha
Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya kinalaani vikali kitendo cha mwandishi Rashid
Mkwinda kupigwa, kujeruhiwa na kuharibiwa zana zake za kazi wakati akitimiza
wajibu wake, kikiamini kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kistaarabu hata kidogo,
kwani ni ukiukwaji mkubwa haki za binadamu na uvunjaji wa Uhuru wa vyombo vya
habari nchini.
Hivyo basi, Chama cha Wandishi wa
Habari Mkoa wa Mbeya kinakitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya kutoa
tamko kuhusiana na tukio hilo, kikielezea hatua zilizochukuliwa kuiadhibu timu
ya Njombe FC kwa kitendo cha kumpiga mwandishi wa habari.
Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa
Mbeya pia kinalitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuchukua hatua
kwa mujibu wa kanuni na sheria za soka nchini dhidi ya wahusika ili kuhakikisha
matukio ya aina hiyo hayajirudii mahali popote nchini.
Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa
Mbeya kinajiuliza sababu za mchezo huo kufanyika bila ya kuwepo kwa ulinzi wa
aina yoyote uwanjani hapo, kwani tunaamini kuwa mchezo huo ulistahili kupewa
ulinzi wa Polisi kwa mujibu wa sheria za nchi, kwa sababu huwenda uwepo wa
ulinzi uwanjani hapo ungepunguza ukubwa na athari za vurugu hizo.
Mwenyekiti Katibu
……………………
………………………….
Nakala kwa:
1.
Umoja wa Club Tanzania (UTPC)
2.
Baraza la Habari Tanzania (MCT)
3.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
4.
Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)
5.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
6.
Njombe FC
7.
Kimondo FC
8.
Vilabu vya Wandishi wa Habari vya Mikoa yote Tanzania
9.
Vyombo vya Habari
Mwisho.
Innocent Mwashambwa
Mratibu-Mbeya Press Club
0768-484383
innoray30@gmail.com
innocentmwashambwa@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment