Na Magreth Kinabo-MAELEZO
Serikali imesema itaendelea kudumisha na kuimarisha
mahusiano ya kideplomasia kati ya nchi rafiki na wadau wa maendeleo ili
kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na
kutimiza malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu wa Milinea (MGDs)
ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni hatua ya kuhakikisha inapunguza kiwango cha umasikini na kuboresha maisha ya watu nchini.
Hayo yalisemwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya
kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 iliyoshirikisha mabalozi mbalimbali
wanazoziwakilisha nchi zao hapa nchini iliyofanyika leo jioni Ikulu
jijini Dar es Salaam.
“Hivi sasa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Bara umekwisha. Ni wakati wa
kufanya kazi na kauli mbiu yangu ni “Hapa Kazi Tu”. Serikali mpya ya
Awamu ya Tano imekuja na mkakati wa kuboresha na kuimraisha utendaji
kazi katika Utumishi wa Umma ili kusisitiza nidhamu na utendaji kazi,
kuhesimu haki za binadamu, utawala bora na kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania wanapata maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii,”alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga aliongeza kwamba Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameiacha nchi
ikiwa imara na marafiki wengi, pia uchumi wake umekuwa katika kiwango
cha asilimia saba (7) kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi za ushirikiano na misaada
yao, hivyo aliwashukuru kwa michango yao waliyoifanya hapa nchini.
“Ninawaomba muendelee kutusaidia kwa kuwa hivi sasa tuna mipango ya
maendeleo ambayo ina lenga kuboresha maisha ya Watanzania wote hususan
wale wanaoishi katika kiwango cha chini cha umasikini,”alisema Balozi
Mahiga.
Alizitaja changamoto kubwa zilizopo katika kutimiza malengo hayo ni
kuwepo kwa hali ya umasikini nchini, ukosefu wa ajira na rushwa. Hivyo
Serikali inafanya kila jitihada za kukabiliana na changamoto hizo kwa
kuwa bila ya kufanya hivyo itakuwa ni vigumu kutimiza malengo ya nchi ya
kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Balozi Mahiga alisema kwamba ili kutimiza malengo hayo, Serikali hivi
sasa inaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali, kujenga
nidhamu, uwazi na uwajibikaji katika matumizi hayo ndani ya Serikali na
hata kwa sekta binafsi na kuimarisha maeneo ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Serikali imesema kwamba itaendelea kuendeleza ushirikiano huo,
ili kuweza kupambana na vitendo vya rushwa, biashara haramu ya binadamu,
ugaidi na matumizi ya silaha.
“Tunawaomba mtusaidie husasan kwenye eneo la upatikanaji wa taarifa,
kujenga uwezo na masuala ya kiufundi katika kukabiliana na vitendo
hivi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu suala la Uchaguzi wa Zanzibar, Balozi Mahiga alisema
Zanzibar inajitegemea katika masuala ya kisiasa na kiutamaduni licha ya
kuwa ni sehemu ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Mahiga alifafanua kuwa Zanzibar ina Katiba yake, Serikali na Tume
Huru ya Uchaguzi .Hivyo kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25, 2015 ulifutwa kwa sababu mbalimbali kama ilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC).
Aliongeza kwamba mazungumzo ya
kufikia muafaka wa suala hilo, yanaendelea ma uchaguzi mwingine
utafanyika Machi 20, mwaka huu. Hivyo mazungumzo hayo bado yanaendelea
ili kuufanya uchaguzi huo uwe huru, haki na uwazi ili kukidhi viwango
vya kimataifa vya demokrasia.
0 comments:
Post a Comment