Pages

Ads 468x60px

Wednesday, August 3, 2016

Mama Kanumba azindua “Kanumba Star Search”

index 
Mshiriki Mkuu wa Shindano la Kanumba Star Search, Florence Mutegoa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya AM Arts Promotion pamoja na Mdhamini wa Shindano la “Kanumba Star Search” kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo tarehe 03.08.2016 Jijini Dar es Salaam,

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mshiriki Mkuu wa Shindano la Kanumba Star Search, Florence Mutegoa (Mama Kanumba) amezindua shindano la kusaka vipaji vya waigizaji watakaoigiza filamu itakayoenzi maisha ya Marehemu Steven Kanumba.
Uzinduzi huo umefanywa leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambapo Mshiriki Mkuu wa Shindano hilo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kudhamini shindano hilo litakaloibua vipaji vipya vya uigizaji.
“Tunatambua thamani ya maigizo ndio sababu tumeamua kuanzisha shindano hili ili kuibua vipaji vilivyojificha, hivyo tunawakaribisha wananchi wote wenye uwezo wa kuigiza waje washiriki kwenye mashindano yetu pia tunaomba wadhamini kujitokeza zaidi ili watusaidie kufanikisha shindano hili”, alisema Mutegoa.
Mutegoa amefafanua kuwa shindano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Kanumba the Great Film na Kampuni ya AM Arts Promotion ambapo hadi sasa shindano hilo lina mdhamini mmoja kutoka Kampuni ya simu za mkononi za KZG – Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AM Arts Promotion, James Mwombeki amesema kuwa marehemu Kanumba alikuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza nchi kimataifa pamoja na kuibua vipaji vya wasanii wa maigizo hivyo hatuna budi kumuenzi kwa kuiendeleza Sanaa ya uigizaji.
“Sisi kama AM Arts Promotion tumeamua kushirikiana kwa pamoja na Mama Kanumba kufanya shindano hili kwa nia ya kuendeleza tasnia ya filamu nchini kama vile marehemu Kanumba alivyokua akijitahidi kuwapa fursa ya uigizaji watu wa kila rika”, alisema Mwombeki.
Naye, Msanii wa filamu, Mayasa Mrisho amewasisitiza wananchi kushiriki kwa wingi kwenye mashindano hayo kwani Sanaa ya uigizaji ni njia mojawapo ya kujipatia kipato na kuinua maisha ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mkononi za KZG – Tanzania, Raymond Kalikawe amesema kuwa wamekubali kuwa wadhamini wa shindano hilo kwa kuwa ukuzaji wa vipaji vya wasanii wa maigizo ni jambo muhimu pia amewaomba wadhamini wengine kujitokeza zaidi kusaidia shindano hilo.
Shindano hilo linatarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu, litaanzia Mikoa ya Kanda ya ziwa na baadae kuendelea katika Mikoa mingine.Washindi wataigiza filamu ya kumuenzi marehemu Kanumba itakayojulikana kama “Maisha ya Kanumba.

0 comments:

Post a Comment