Na Beatrice Lymo-
MAELEZO
“Uhai wa wanyamapori
ni jambo linalotuhusu sisi sote katika Afrika, viumbe hai wa porini wakiwa katika
mapori waishimo sio muhimu tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni
sehemu ya maliasili yetu na mustakabali wa maisha yetu baadaye”
Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alisema hayo wakati akitoa tamko la Arusha kuhusu Uhifadhi wa
wanyamapori kipindi Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961.
Alisema kwa kukubali
dhamana ya wanyamapori, watanzania watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wajukuu
na watoto wa kitanzania wanaweza kufurahia urithi mkubwa wa thamani hiyo adimu
ya wanyamapori.
Juhudi za uhifadhi na
kulinda rasilimali, malikale na kuendeleza shughuli za ufugaji nyuki pamoja na
kukuza Sekta ya Utalii ikiwa ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii
zilikuwepo hata kabla ya ukoloni ambapo jamii nchini zilitenga mapori kwa ajili
ya kuabudia na kutambika.
Kuingia kwa wakoloni
nchini kuliambatana na kutunga Sheria za uhifadhi wa rasilimali za maliasili na
malikale ambapo ni Sheria ya kuhifadhi Majengo ya kihistoria ya mwaka 1937,
Sheria ya Makumbusho ya mwaka 1941, Sheria ya Usimamizi wa Misitu ya mwaka
1957, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959, Sheria ya Hifadhi za Taifa
ya mwaka 1959 na Sheria ya kuhifadhi wanyama ya mwaka 1959.
Chini ya uongozi wa
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia mwaka 1961 Wizara ya Maliasili na
Utalii imekuwa na Sera na Sheria tofauti kulingana na mabadiliko yaliyokuwa
yakitokea duniani katika nyanja za kiuchumi, kiteknolojia, kiasiasa na kijamii.
Juhudi za Baba wa
Taifa katika kuhakikisha Sekta ya utalii ambapo ilikuwa na idara moja mwaka 1961 kuanza kuwa na Sera
ya uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii nchini zinaonekana.
Mabadiliko na matukio
makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya uhuru mwaka 1961
yalipelekea jitihada za makusudi za kuwezesha wazawa kielimu ili kuweza
kuchukua nafasi za utendaji na uongozi ambazo awali zilishikiliwa na wageni.
Aidha, mwaka 1967
kufuatiwa kupitishwa Azimio la Arusha chini ya uongozi wa Baba wa Taifa mali
binafsi zilitaifishwa na kuundwa kwa mashirika na taasisi za umma ambapo Wizara
iliunda mashirika ya umma ikiwemo Shirika la Wanyamapori, Shirika la Viwanda
vya mbao, Shirika la Utalii Tanzania, Shirika la kuhudumia wasafiri na Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kukuza na kuimarisha sekta ya utalii
nchini.
Katika mabadiliko hayo
ndani ya Wizara, juhudi za Mwalimu Nyerere zilipelekea Serikali kujitoa katika
kuendesha shughuli za kibiashara na kujikita katika kusimamia Sera na
uwezeshaji.
Kadhalika katika
suala la ulinzi wa rasilimali za maliasili, Serikali ilirithi mfumo wa ukoloni
ambapo Serikali ilikuwa ndiye mlinzi na mwendelezaji mkuu wa rasilimali za
maliasili, malikale na utalii ambapo mabadiliko ya kisera na mwelekeo wa
uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali ulifanyika miaka ya 1991 kwa kuhimiza
ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za
maliasili, malikale na utalii.
Ushirikishwaji jamii
katika shughuli za maliasili na utalii ulichangia katika Wizara kuanzisha vitengo mbalimbali ikiwemo
kitengo cha Ugani katika idara na taasisi zake ikiwa na lengo la kuimarisha na
kukuza sekta ya utalii nchini.
Vilevile, katika
suala la ajira na jinsia katika wizara, wakati nchi inapata uhuru sekta za maliasili hususani wanyamapori,
misitu, malikale na nyuki zilikuwa maalumu kwa wanaume ambapo juhudi za Mwalimu
Nyerere ziliwezesha kupatikana kwa ajira ikihusisha jinsia zote mbili, ambapo
sekta ya utalii ikaajiri mwanamke kwa mara ya kwanza mwaka 1970.
Katika sekta ya nyuki
wanawake wawili waliokuwa na astashahada ya ufugaji wa nyuki waliajiriwa mwaka
1975, sekta ndogo ya misitu iliajiri mwanamke wa kwanza mwenye shahada mwaka
1976, katika sekta ndogo ya wanyamapori mwanamke aliajiriwa mwaka 1967 na
katika sekta ya mambo ya kale mwanamke aliajiriwa mwaka 1978 kwa ngazi ya cheti
na 1981 kwa ngazi ya shahada.
Kama Mwalimu Nyerere,
Rais John Pombe Magufuli naye ameonyesha kukerwa na vitendo vya ujangili na
biashara haramu ya kuuza meno ya tembo. Katika hotuba zake Mhe. Rais Magufuli
amekuwa akisisitiza utunzaji wa maliasili kwa ajili ya maendelo ya Taifa.
Pia katika kuongeza
tija na kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa zilizofanyiwa utafiti, wizara
ilianzisha vyuo vya ulinzi, uhifadhi na uendelezaji wa maliasili, malikale na
utalii ambapo chuo cha viwanda vya misitu kilianzishwa mwaka 1975, chuo cha
ufugaji nyuki Tabora mwaka 1978 pamoja na vyuo vya elimu ya wafanyakazi Rongai
na Sao Hill vilivyoanzishwa mwaka 1979 kwa lengo la kutoa elimu ya awali ya
uoteshaji miche na kuhudumia misitu.
Katika kukuza na
kuimarisha sekta ya utalii nchini Mwalimu Nyerere aliweza kutekeleza majukumu
ya wizara kulingana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea nchini na duniani
katika nyanja ya kiuchumi, kisiasa kiteknolojia na kijamii.
Juhudi hilo
zilipelekea wizara kuongeza vituo vya malikale na kutangaza maeneo tofauti kama
urithi wa Taifa, mashamba ya miti yaliongezeka, misitu ya asili pamoja na
hifadhi za Taifa kuongezeka.
Mbali na hayo juhudi
za Mwalimu katika kukuza na kuimarisha sekta ya utalii mara baada ya uhuru zilichangia
katika ongezeko la mikusanyo ya malikale ambapo wakati wa uhuru wizara
ilihifadhi jumla ya mikusanyo 10,151 ya fani za Akiolojia, mila, historia,
bayolojia na nyaraka mbalimbali.
Aidha baada ya uhuru
kutokana na tafiti zilizofanywa na watafiti wazawa na wageni kutoka nje ya nchi
hadi juni, 2011 wizara imefanikiwa kuhifadhi nchini urithi wa malikale
unaohamasisha wenyeji jumla ya mikusanyo 337,361.
Katika suala la
ongezeko la idadi ya watalii wanaongia nchini ndani ya uongozi wa Mwalimu
Julius Nyerere idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 9,847 mwaka 1960
hadi watalii 103,361 mwaka 1986.
Mbali
na hayo katika kuendeleza jitihada za kukuza na kuimarisha sekta ya utalii
nchini, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, kwenye Sherehe ya kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru, wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya Baba Wa Taifa, Mwalimu
Julius K. Nyerere, Singida mwaka 2005 alisema kuwa sekta ya utalii ni muhimu
katika ukuzaji wa uchumi wetu hivyo ni budi kuitunza na kuithamini.
“Ukweli
unaojionyesha ni kwamba kama tukijikita katika sekta hii tunaweza kuongeza kasi
ya ukuaji wa uchumi katika nchi yetu, nategemea kwamba sekta hii inaweza
ikatuongezea mchango wake katika pato la Taifa hivyo tutumie rasilimali
zilizopo kuwavutia watalii na wawekezaji wengine kuingia katika sekta hii”,
aliongeza Rais Mkapa.
Alibainisha
kuwa hifadhi ya mazingira ni eneo ambalo
linahitaji nguvu za pamoja na za haraka katika kuepusha athari zinazoweza
kutokea kama hatujali na kutilia maanani hivyo jamii inahitaji kuhifadhi misitu, vyanzo vya maji na kupanda miti kwa
wingi ili kuzuia nchi kuwa jangwa.
Kwa upande wake Rais
Mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali Hassan
Mwinyi hivi karibuni alitoa wito kwa
watanzania kuongeza juhudi katika kusaidiana na Serikali kupiga vita ujangili
hapa nchini kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo.
Rais mstaafu huyo,
alisema kumekuwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori hapa nchini ambayo ni
dhambi na ni kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao wana haki ya
kuishi kama viumbe wengine.
“Kumekuwa na matukio
mengi ya uuaji wa wanyamapori ikiwemo tembo na faru na hivyo kupunguza rasilimali
ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo hicho ni kinyume na kusudio la Mungu
hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda, kuwaendeleza na kuwalinda wanyama hao
kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia pato la Taifa” aliongeza Rais Mstaafu Mwinyi.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika sherehe za miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar aliwataka Wananchi kutumia vivutio vya utalii vilivyopo ili
kuweza kukuza utalii wa ndani kwani kwa pamoja taifa litaendeleza juhudi za
kukuza sekta ya utalii kwa kauli mbiu ya “Utalii kwa wote” ili iendelee kuwa na
mchango mkubwa katika soko la ajira, kuingiza fedha za kigeni na katika kukuza
Pato la Taifa kwa jumla.
Sambamba na hilo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema asilimia 80ya
mapato ya fedha za kigeni zinazoingia nchini kupitia Sekta ya Utalii inaweza
kubakia kuwa ndoto kama suala la amani na utulivu halitazingatiwa na kupewa
nafasi yake chini ya usimamizi wa Jamii kwa mashirikiano na Serikali Kuu.
Alisema hakutakuwa na
mgeni wala mtalii atakayekuwa na shauku ya kutaka kuingia nchini sambamba na
kufifia biashara ya Utalii endapo amani na utulivu uliopo utachezewa na hatimae
kutoweka kabisa.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa kumekuwa na
changamoto zilizohusu masuala ya Maliasili na Utalii zilizojitokeza wakati wa
kampeni ikiwemo ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya
mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato hivyo kuahidi kuzifuatilia
changamoto hizo ili kuweza kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Mbali na hayo wakati akitoa
hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Jamhuri Rais Magufuli aliwataka mabalozi
wanaowakilisha Tanzania nchi za nje kutumia fursa walizo nazo katika kutangaza
utalii wa nchi ili kuweza kuongeza pato la Taifa.
Wizara ya Maliasili
na Utalii inaendelea kutekeleza majukumu yake licha ya mabadiliko na changamoto
mbalimbali na inatarajiwa kuwa rasilimali za maliasili, malikale na utalii
zitaendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa juhudi za kukuza uchumi wa Taifa.
Hakika Mwalimu
Nyerere mchango wake kwa sekta ya utalii haiwezi kusahaulika, itakumbukwa
vizazi hadi vizazi. Utalii ukitiliwa mkazo na kuboresha miundombinu ya
kuwawezesha watalii kufika na kukaa bila taabu ni dhahiri watalii wataongezeka
na hivyo kukuza Pato la Taifa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment