Kuoa au kuolewa kunabadilisha uhusiano
wako na wazazi wako.NA:MWL C.MWAKASEGE
Mwanzo.2:24 anasema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama
yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili moja”. Ukiangalia
(Zaburi.45:10-11) anasema, “Sikia binti utazame (maana yake anazungumza
na msichana) utege sikio lako. Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako
na mfalme atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako naye
umsujudie”.
Najua watu wengi sana wanataka waingie kwenye ndoa, waoe
au waolewe, lakini uhusiano wao na wazazi wao usibadilike, haiwezekani.
Biblia imeweka wazi kabisa, unataka kuoa, mwanamume lazima kwanza
aachane na baba yake na mama yake, maana yake kuna mabadiliko. Kuna
mabadiliko mahali pakuishi, kuna mabadiliko juu ya mtazamo wako wa
kwanza wa maisha yako. Mke wako hawezi kuwa mama yako, na mume wako
hawezi kuwa baba yako. Mke wako anakuwa mke wako na si mama yako. Mume
wako anakuwa mume wako na si baba yako.
Na kabla hujafikia maamuzi
ya namna hiyo – ukiingia kwenye ndoa, ndoa yako itakuwa ngumu. Maana
inawezekana unaishi vizuri na wazazi wako, kiasi ambacho maamuzi yako
yoyote unayofanya lazima ushirikiane nao, na hiyo ni hatua nzuri kabisa.
Lakini ukiishaingia kwenye ndoa, mtu wa kwanza wakushirikiana naye ni
mke wako kama umeoa, na ni mume wako kama umeolewa lakini, sio baba
yako, sio mama yako.
Na wazazi wengine wasingetaka kuona kwamba
unakuwa mbali nao kwa jinsi hii, wanataka waendeleze maamuzi yao na
utawala wao waliokuwa nao juu yako mpaka kwenye ndoa yako, haiwezekani.
Biblia inakataa. Sasa ukisoma ile Mwanzo unaweza ukafikiri ni wanaume tu
wakioa ndio wanatakiwa watoke, waachane na wazazi wao, lakini Zaburi
45:10,11 inatuambia wazi kabisa, inasema, “Sikia, binti, utazame, utege
sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. Naye Mfalme
atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie”.
Sasa
haimaanishi usiwasalimie, haimanishi usiwasaidie, lakini ningekuwa
nazungumza kwa kiingereza ningekuambia, “your priorities must change”
lazima ubadilike jinsi ambavyo unaweka kipaumbele katika watu ulio nao.
Unapoamua kuolewa, wa kwanza sio baba yako wala sio mama yako, wa
kwanza ni mume wako baada ya Yesu. Katika mahusiano ya kibinadamu
anayekuja pale wa kwanza baada ya Yesu moyoni mwako ni mume wako. Ikiwa
hujafikia maamuzi ya namna hii moyoni mwako basi bado hujafikia utayari
wa kuolewa. Na ina madhara yake magumu. Maana biblia inasema, kabla
hujawasahau watu wako na watu wa nyumba ya baba yako, mume wako hawezi
kuutamani uzuri wako, ukitaka autamani uzuri wako lazima uwasahau kwanza
watu wa nyumbani kwa wazazi wako.
Sasa kuna tofauti ya kupenda na
kutamani. Kabla hujaolewa au kabla hujaoa huruhusiwi kutamani. Lakini
ukiisha oa unaruhusiwa kutamani lakini mke wako tu. Ukiishaoa kutamani
mke wako ruksa, na biblia imeweka vizuri kabisa, na ukiishaolewa
kutamani mume wako ni ruksa. Lakini biblia imeweka utaratibu wa ajabu
sana kwamba, ili mume amtamani mke wake, lazima mke wake awasahau kwanza
watu wa nyumbani mwa wazazi wake. Hiki ni kigezo kigumu sana.
Ndio
maana unaweza ukakuta mtu ana mke mzuri sana lakini hamtamani. Unaweza
ukafikiri labda ni kwa kuwa hajajipamba vizuri; lakini hata kama
atajipamba, atajikwatua kuanzia asubuhi mpaka jioni, – anaweza hata
akatumia muda mwingi kwenye kioo kuliko kwenye maombi akijitengeneza,
lakini bado mume wake asimtamani; kwa nini? Kwa sababu ndani yake
hajaachia watu wa nyumba ya wazazi wake. Au watu wa nyumba ya baba yake
wana nafasi kubwa moyoni kuliko mume wake.
Ni mabadiliko ambayo
lazima uyatarajie, watu wengi sana huwa hawafikirii hayo, wanafikiri ni
kitu rahisi. Unaweza sasa ukaelewa kwa nini watu wengine ikifika siku
ile ya “send off”, yaani ya kum’send’ msichana ‘off’ asikae tena
nyumbani kwa baba yake, hiyo siku ni ngumu sana kwa wazazi. Kwa sababu
wanajua, wanaagana na msichana wao, mahusiano yao waliokuwa nayo toka
mwanzoni, tangu alipozaliwa, alipokuwa tumboni mpaka wakati huo
yanabadilishwa, yanajengwa mengine, sasa anakwenda kuwa mke wa mtu,
hawawezi tena kuingilia maamuzi juu yake, amefunga agano mahali pengine.
Unakuta siku hiyo wazazi wengine wanalia, unakuta vijana wengine
wanalia, wasichana wengine wanalia. Usije ukafikiri ni kitu rahisi.
Ndani ya nafsi kuna vitu vinaachana, kati ya wazazi na wale watoto
wanaoana.
Tuesday, October 16, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment