Marehemu Bi Kidude alikuwa ni gwiji wa
muziki katika Bara la Afrika. Jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. Bi Kidude
ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki wa mwambao ambao
hujulikana kwa jina la Taarabu.
Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi
za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrikaumekita sana katika mwambao wa Afrika
Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na
kwingineko.
Leo hii ni Marehemu! Nguli na Mtunukiwa wa Nishani
ya Uhuru wa Tanganyika/Tanzania 2012, Fatuma binti Baraka au Bi Kidude,
alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba
(7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la
kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude aliwahi kusimulia kuwa hafahamu tarehe
halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa
wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu
ya Kwanza ya Ulaya. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo
wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka
90.
Bi Kidude aliendelea kusema uimbaji aliuanza tangu
alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na
aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu
mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude
na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani
kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje,
kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa
akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo
hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka
nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa
kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo
nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua
kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara
sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya
1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake
uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani
pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe,
pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu
mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika
wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa
mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo
mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na
tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani
ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya
kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na
kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si
kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya
kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo
ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa
ni pamoja
na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha.
Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa
Jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine
zaidi ya Kurani.
Bi Kidude pia amekuwa akishirikishwa na wasanii
wengi wakongwe na chipukizi katika nyimbo zao. Miongoni mwa nyimbo zinazotamba
sana siku hizi ambazo Bi Kifude ameimba na vijana wa kisasa ni za Msanii Ali
Toll maarufu AT.
Mbali na AT lakini pia Bi Kidude amewika na kung'ara
zaidi katika wimbo mwingine wa vijana wa Ahmada Umelewa wa Msanii Offside Trick
ambao umepigwa marufuku kupigwa kwa sasa visiwani
Zanzibar.
R.I.P FATUMA BARAKA “BI KIDUDE”..
0 comments:
Post a Comment