Pages

Ads 468x60px

Wednesday, August 21, 2013

RWANDA NA UGANDA WAJITOA BANDARI YA DAR ES SALAAM



Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa), kimesema Rwanda na Uganda zitajitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu.

Katibu Mtendaji wa Tatoa, Zacharia Hanspope aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa nchi hizo zinajitoa kutokana na matatizo mbalimbali ambayo kwa muda mrefu zimekuwa zikiyalalamikia lakini Serikali haikuchukua hatua.

Hanspope alisema ushuru wa barabara na ushuru wa forodha ni baadhi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara mbalimbali wa nchi hizo.

“Serikali ipunguze gharama za ushuru wa barabara na ushuru wa forodha ili kuwa na ushindani sawa na bandari nyingine na hivyo kuzivutia kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Hanspope.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary Chambo alikataa kuzungumzia lolote kuhusu suala hilo akisema halina mantiki yoyote kwake.... “Hivi hilo jambo unaloniuliza lina sense (mantiki) yoyote? Mie siwezi kujibu lolote nenda ukamuulize mwenyewe (Hanspope) maana wakati akisema mimi sikuwepo.”

Alisema kujitoa kwa Rwanda na Uganda kuitumia Bandari ya Dar es Salaam hakutakiathiri chama hicho tu, bali uchumi wa taifa kwa ujumla.

Hayo yanatokea wakati Rwanda ikiendeleza vita yake ya maneno na Tanzania na mfululizo wa matukio ya kuitenga Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Viongozi wa Kenya, Rwanda na Uganda walikutana Juni 25, mwaka huu mjini Entebbe, Uganda na kukubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara baina yao.

0 comments:

Post a Comment