Pages

Ads 468x60px

Sunday, February 7, 2016

Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe




·        
Kipunji Nyani adimu duniani
Ni hifadhi inayopatikana katika Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Ilihifadhiwa Mwaka 1949 kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji na baionuai (biodiversity). Ukubwa wake ni hekta 13,652.1. Hifadhi hii ipo umbali wa km 25 kusini Mashariki mwa mji wa Mbeya na umbali wa km 7 kaskazini mwa mji wa Tukuyu
·          
      Hifadhi Asilia ya Mlima Rungwe inamilikiwa na serikali kuu chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Usimamizi wake uko chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Wakala huu ulianzishwa mwaka 2010 kwa ajili ya kusimamia rasilimali za misitu na nyuki kwa tangazo la serikali na. 269 la tarehe 30/07/2010
·        
       Baada ya kuona umuhimu mkubwa wa hifadhi ya Mlima Rungwe, mchakato wa kupandisha hadhi ulianzishwa mwaka 2008 na hatimaye mwaka 2009 hifadhi ilipandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Mazingira Asilia. Hifadhi ya Mazingira Asilia ni hadhi ya juu kuliko Msitu wa Hifadhi. Hifadhi ya Mazingira Asilia hairuhusu matumizi mengine zaidi ya elimu, utafiti na utalii.
·          
      Katika kusimamia Hifadhi ya Mazingira Asilia, msimamizi ni Mhifadhi Mkuu (Conservator)
Kipunji stealing maize cobs
ambaye huripoti kwa Meneja wa Kanda. Mhifadhi Mkuu anasaidiwa na Maafisa Misitu ambao wako katika vituo vya Syukula, Kandete, Tukuyu na  Unyamwanga.
·        
             Kwa Tanzania, kuna hifadhi 11 tu zenye hadhi ya Mazingira Asilia ambazo ni Mlima Rungwe, Kilombero (Iringa), Uzungwa (Iringa), Uluguru (Morogoro), Mkingu (Morogoro), Rondo (Lindi), Amani (Tanga), Chome (Kilimanjaro), Nilo (Tanga), Minziro (Kagera) na Magamba (Tanga).
·         Hifadhi ya Mlima Rungwe imezungukwa na Vijiji 23 kama inavyooneshwa hapa chini. Hatahivyo vijiji vinavyogusa hifadhi moja kwa moja ni 16 tu.

Vijiji vinavyozunguka Hifadhi Asilia Mlima Rungwe
Kijiji
Kata
Tarafa
Idadi ya watu
(sensa ya 2002)
Idadi ya watu ( sensa ya 2012)
Mabadiliko %
1
Bujingijila
Kandate
Busokelo
828
872
5
2
Ndala
Kandate
Busokelo
2 541
1 777
-43
3
Lugombo
Kandete
Busokelo
934
781
-20
4
Katumba
Katumba
Pakati
5 255
6 452
19
5
Ibumba
Suma
Pakati
1 165
1 136
-3
6
Masebe
Katumba
Pakati
1 255
1 375
9
7
Kabale
Suma
Pakati
998
909
-10
8
Ngumbulu
Isongole
Ukukwe
115
1 107
90
9
Ilundo
Kiwira
Ukukwe
4 051
4 694
14
10
Nditu
Suma
Ukukwe
2 391
2 415
1
11
Syukula
Kyimo
Ukukwe
4 653
4 461
-4
12
Ikama
Katumba
Ukukwe
1 682
1 415
-5
13
Ndwati
Isongole
Ukukwe
431
392
-10
14
Mpandapanda
Kiwira
Ukukwe
6 308
8 356
25
15
Isyonje
Isongole
Ukukwe
1 631
1 389
-17
16
Ndaga
Isongole
Ukukwe
4 044
5 056
20
17
Mbeye one 
Isongole
Ukukwe
961
1 167
18
18
Kibisi
Kyimo
Ukukwe
1 728
1 678
-3
19
Ilolo
Kiwira
Ukukwe
3 891
3 239
-20
20
Unyamwanga
Isongole
Ukukwe
1 502
1 372
-9
21
Ntokela
Isongole
Ukukwe
3 390
6 438
47
22
Idweli
Isongole
Ukukwe
1 864
1 768
-5
23
Suma
Suma
Ukukwe
976
839
-16
Jumla
52, 594
59 ,091


Umuhimu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe
  1. Chanzo cha maji (mito inayo tiririka kutoka kwenye hifadhi)
Mito hii ina umuhimu mkubwa kwa vijiji na miji kadhaa kama Katumba, Kiwira, Kandete na sehemu zingine. Mito hii ni kama; siniki, marogala, kipoki, kilasi, Mulagala na mingineyo ambayo maji yake yanaingia Ziwa Nyasa. Imefahamika kuwa mito hii huchangia asilimia 48 ya maji ya ziwa Nyasa. Aidha kilimo katika bonde la ziwa Nyasa hutegemea sana maji kutoka hifadhi hii
2.     
       Kurekebisha Hali ya hewa
Uwepo wa hifadhi hii umepelekea kuwa na hali ya hewa safi ndani ya wilaya ya Rungwe na maeneo mengine ambayo imechujwa na mimea, pia inachangia kuvuta mvua za kutosha kama matokeo ya uhifadhi wa mazingira ukilinganisha na sehemu zingine ambako kuna uhaba wa misitu na kama ipo haitunzwi ipasavyo
3.      Uchumi kutokana na Utalii

Kutokana na sifa za kipekee za Hifadhi  ya Mazingira Asilia ya Mlima Rungwe: ikiwemo urefu wa mlima, mashimo ya volukano (paluvalutali, Lusiba na Ng’ombe) na wanyama aina ya kipunji, na maji moto. Vyote hivi vimekuwa vinashawishi watalii kutembelea hifadhi yetu ya mazingira asilia ya mlima Rungwe. Pia hifadhi imepakana na hifadhi ya Kitulo ambayo ina vivutio vingi vya kitalii
4.       
      Hifadhi ya baionuai muhimu
5.      Huchangia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Kazi zinazofanyika katika kuhifadhi
Katika kuhakikisha kuwa hiafadhi hii inabakia kuwa katika hali ya kuridhisha, shughuli mbalimbali hufanyika ikiwa ni pamoja na;
i.                    Kusafisha mipaka, kazi hii inafanyika kila mwaka wakati wa kiangazi. Hii inasaidia kuzuia uvamizi hasa unaotokana na shughuli za kilimo
ii.                  Doria za mara kwa mara. Kazi hii hufanyika kwa kushirikisha kamati za Mazingira za Vijiji, skauti na vyombo vya usalama
iii.                Utoaji wa elimu. Lengo la kazi hii ni kuongeza uelewa kwa jamii inayozunguka hifadhi ili iendelee kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira.
iv.                Uwekaji wa alama za kudumu kwenye mipaka na njia za kuingilia kwenye hifadhi. Alama hizi ni pamoja na maboya (beacons), mabango na mahandaki ya uelekeo (directional trenches)
v.                  Uanzishaji wa vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya jamii inayozunguka hifadhi

Mapato kutoka katika hifadhi Mazingira Asilia Mlima Rungwe
Kama ilivyoelezwa awali kuwa hifadhi hii ni kwa ajili ya mafunzo, utafiti, na utalii ikolojia tu. Hakuna uvunaji wowote ule unaofanyika. Kwahiyo hifadhi hii inapata mapato kutokana na ada za utafiti na za utalii tu. Kwa mfano katika kipindi cha Februari 2014 hadi Juni 2015 utalii uliingiza kiasi cha TSH 6,007,655/- kiasi ambacho ni asilimia 0.7 ya bajeti ya kusimamia hifadhi kwa mwaka mmoja. Asilimia 5 ya makusanyo hupelekwa Halmashauri kwa mujibu wa sheria. Kiasi hiki kinapaswa kupelekwa katika vijiji kupitia halmashauri kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kuhifadhi
Hifadhi yetu hii inakabiliwa na changamoto zifuatazo:
i.                     Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kufanikisha uhifadhi; mfano: kufanya doria za kina na tahadhari ya moto, na tafiti mbalimbali.
ii.                   Upungufu wa vitendea kazi; mfano magari na rasilimali watumishi.
iii.                 Miundo mbinu ya barabara na majengo kwa ajili ya ofisi na watu
iv.                 Miti vamizi (pine)
v.                   Uvunaji haramu wa mbao, mkaa, na mazao mengine ya misitu. Aidha uwindaji haramu wa wanyama kama Kipunji na Minde unafanywa na baadhi ya wanakijiji wasio waaminifu.
vi.                 Moto kutoka kwenye mashamba ya watu, wawindaji na urinaji asali usio fuata utaalam wa kisasa
vii.              Ushiriki usioridhisha kutoka kwa baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi. Baadhi ya vijiji vimekuwa vikikataa kushiriki katika kuhiafadhi hasa shughuli kama za kuzima moto. Hii inatokana na madai kwamba hawaoni faida zinazotokana na hifadhi hii.

Hali Halisi ya Hifadhi ya Mlima Rungwe
Hifadhi Asilia ya Mlima Rungwe imeboreka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kipindi cha miaka 5 iliyopita. Matukio mengi ya uharibifu kwa kukata miti na kilimo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
·         Kwa sasa hifadhi hii ina tatizo la uvamizi wa miti ya kigeni (Pinus patula). Miti hii iliripotiwa na WCS kwa mara ya kwanza mwaka 2004 ikiwa imevamia hekta 64. Hadi sasa eneo ililovamiwa ni zaidi ya hekta 100.
·         Matukio ya moto. Hili ni tatizo kubwa ambalo huathiri hifadhi kwa kiasi kikubwa sana. Uoto wa asili na wanyama hasa wado wadogo hupotea. Mwaka 2009 moto uliteketeza takribani hekta 2,000 za uoto hasa ukanda wa nyasi (grasslands). Mwaka 2015 moto uliteketeza takribani hekta 1,200 ambao pia uliteketeza eneo la nyasi. Vyanzo vya moto katika hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe ni uwindaji na kilimo.

Upekee wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe
·         Hifadhi Asilia ya Mlima Rungwe ni ya kipekee kwa kuwa na uoto aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na msitu wa mlimani (lower and upper montane forests), ukanda wa mianzi (bamboo belt), heathland, mchanganyiko wa miti mifupi na nyasi (woodland), na nyasi (grassland).
·         Ni sehemu ambayo sampuli ya nyani apatikanaye Tanzania pekee (Rungwecebus kipunji) ilichukuliwa na hivyo nyani kupewa jina la Rungwe kwa ukumbusho huo
·         Volkano iliyotulia yenye mashimo ya kuvutia (volcanic craters)
·         Ni Mlima wa tatu kwa urefu Tanzania ukiwa na urefu wa meta 2,981 baada ya Kilimanjaro (5595m) na Meru (4,600m).
·         Makazi ya vinyonga wenye pembe tatu wapatikanao katika hifadhi hii pekee


Washirika katika kuhifadhi Msitu Mazingira Asilia Mlima Rungwe
Hifadhi Asilia ya Mlima Rungwe inapata michango ya kihifadhi kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile;
1.      Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori na Mazingira (Wildlife Conservation Society). Shirika hili limekuwa likifanya kazi mbalimbali za kuhifadhi Mlima Rungwe tangu miaka ya 2003. Shiriki hili hufanya kazi mbalimbali hasa za utafiti, utoaji elimu kwa jamii na kusaidia miradi mbalimbali ya kuongeza kipato kwa jamii inayozunguka hifadhi. Shughuli hizo ni pamoja na miradi ya ufugaji nyuki, upandaji miti n.k
2.      SPANEST (Strengthening Protected Areas Network for Southern Tanzania).
3.      HIMARU (Hifadhi Mazingira Rungwe)
4.      African Wildlife Foundation (AWF). Shirika hili kwa sasa linasaidia kutengeneza mpango wa Usimamizi (Management Plan) wa Hifadhi hii.
5.      Jamii zinazozunguka hifadhi
6.      Halmashauri ya Wilaya Rungwe
7.      GEF/UNDP. Haya ni mashirika ya kimataifa ambayo kwa sasa yametoa ufadhili kupitia mradi unaoitwa “Enhancing Forest Nature Reserves Network for Biodiversity Conservation in Tanzania”. Mradi huu utafadhili shughuli mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa ofisi, utengenezaji wa barabara, njia za kitalii, ununuaji wa vitendea kazi mf. Magari na pikipiki; uwekaji wa mabango n.k.

Mikakati ya baadaye ili kuboresha hifadhi
Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe ina mikakati mbalimbali ili kuboresha uhifadhi wa Msitu wa Hifadhi Mazingira Asilia Mlima Rungwe
1.      Kuboresha miundombinu ya barabara na njia za utalii
2.      Kuingia makubaliano (Joint Management Agreements) na jamii inayozunguka hifadhi ili wajue kwa kina faida za hifadhi hii na baadaye washiriki vizuri zaidi katika kuhifadhi Mlima Rungwe
3.      Kutangaza hifadhi kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na websites, blogs
4.      Kupandisha hadhi kutoka Hifadhi Mazingira Asilia na kuwa Urithi wa Dunia (world Heritage)

Mpango wa kuondoa miti vamizi
Hifadhi hii tayari ina mpango wa usimamizi ambao utaanza kutekelezwa mwaka huu 2016. Katika mpango huu, kuna mpango mdogo wa kuondoa miti vamizi aina ya misindano (Pines) kama ilivyoainishwa awali. Miti ya misindano ni tatizo kubwa katika hifadhi ya Mlima Rungwe kwani inahatarisha ikolojia yake. Tatizo la miti vamizi halipo katika hifadhi hii tu bali katika maeneo mengine kama vile Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.

Katika kutekeleza mpango mdogo wa kuondoa miti vamizi, hatua kadhaa tayari zimefikiwa ikiwa ni pamoja na kuwasilisha andiko (proposal) makao makuu TFS. Katika mpango huo mdogo tunataraji kufuata hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kupima ujazo wa miti na eneo lililovamiwa kasha kutoa elimu kwa jamii inayozunguka hifadhi juu ya kusudio la kuiondoa miti hiyo. Hii itahusisha pia viongozi mbalimbali katika ngazi za kata na wilaya. Shirika la WCS litasaidia katika kufanikisha zoezi hili. Aidha uondoaji wa miti hii unatarajiwa kufaidisha TFS na jamii inayozunguka hifadhi.

0 comments:

Post a Comment