Msajili
 wa Vyama vya Siasa Nchini Mhe. JaJi Francis S.K. Mutungi amevitaka 
vyama vya Siasa nchini kuhakikisha kuwa Katiba na Kanuni za Vyama vya 
Siasa zinaheshimiwa na kufuatwa katika utendaji wa kila siku wa chama 
cha siasa ili kuepuka migogoro na migongano ndani ya vyama.  Hayo 
ameyabainisha kwenye barua yenye Kumb. Na. HA.322/362/01/103 
aliyoiandikia vyama vya siasa mapema leo.
“Nimeona 
ni vyema nitumie fursa hii kuviasa Vyama vya Siasa kuhusu hali hii, 
kwani hali hii ya kufanya mambo kiholela pasipo kufuata Katiba na Kanuni
 kama itaachwa iendelee hivi ndani ya vyama kwa hakika italeta migogoro 
na mipasuko mikubwa ndani ya Vyama vya Siasa husika.”
“Wakati huu ambapo nchi yetu inasubiri marudio ya Uchaguzi Mkuu wa 
Zanzibar, nimeandikiwa barua na pia kupata nakala za barua kutoka kwa 
baadhi ya Vyama vya Siasa kuhusu migongano ya wanachama na viongozi au 
viongozi wenyewe kwa wenyewe kuhusu suala la kushiriki uchaguzi wa 
marudio Zanzibar. “alisema Jaji Mutungi
Barua hiyo ilibainisha  kuwa suala hilo la migongano limejitokeza pia 
kwa wingi kwenye Vyombo vya Habari, ambapo wanachama na viongozi au 
viongozi wenyewe kwa wenyewe wametofautiana na kupingana hadharani.
Jaji 
Mutungi amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 3(1) ya kanuni za Usajili wa 
Vyama vya Siasa za mwaka 1992 (GN.No. 111) Vyama vya Siasa 
vinaposajiliwa vinapaswa kuwasilisha Katiba na Kanuni zake kwa Msajili 
wa Vyama vya Siasa.
“Ikumbukwe
 kwamba, suala la msingi hapa ni kwamba,sharti la kuwepo kwa Katiba na 
Kanuni katika chama, kimsingi ni mwendelezo wa kukuza na kudumisha dhana
 ya kuendesha Vyama kitaasisi kulingana na mwongozo uliokubalika na 
kuasisiwa kichama kwa mfumo wa Katiba na Kanuni za chama na si kuendesha
 chama kiholela kama inavyoelekea kuota mizizi kwa baadhi ya Vyama vya 
Siasa hivi sasa.”ameongeza Jaji Mutungi
 Jaji 
Mutungi amevisihi Vyama vyote vya Siasa, kuhakikisha kwamba matamko ya 
chama hususan yahusuyo msimamo wa chama kuhusu jambo zito la kisera, 
kitaifa n.k., mathalan kama lilivyo la uchaguzi huu wa Zanzibar basi 
yatolewe rasmi na mtu mwenye mamlaka ya kuongea kwa niaba ya chama. Na 
endapo kuna mwananchama au kiongozi ambaye ataenda kinyume achukuliwe 
hatua haraka iwezekanavyo na chama husika kwa kuzingatia   katiba na 
kanuni zake ili kuepusha sitofahamu inayokuwa imejitokeza katika jamii.
“Ni vyema
 misimamo kama hiyo ya chama itokane pia na vikao halali vya chama na 
siyo matakwa ya kiongozi mmoja au mwanachama mmoja au wachache.  
Vinginevyo kama tutapeleka na kufanya uendeshaji wa vyama kiholela 
tutachangia kuwachanganya wananchi na kupoteza kabisa imani na heshima 
ya Jamii iliyokuwa imeanza kujengeka kwa Vyama vya Siasa”. Amesisitiza 
Jaji Mutungi
Aidha 
vyama vvya Siasa vimeaswa kuchua hatua  ya haraka iwezekanavyo kwa 
mwanachama au kiongozi  wa chama anayefanya mawasiliano ama kutoa 
matamko bila idhini ya mamlaka na pia vyama  vimeonywa kutowajengea 
wananchi tashwira ya kwamba kuna makundi yanagombania madaraka  na 
kuendeleza maslahi binafsi  kwa sababu jambo hilo linashusha hadhi ya 
vyama vya Siasa nchini.
 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment