MKUU wa
Wilaya ya Mbozi, Mkoani, Dk. Michael Kadeghe, amesema kuwa asilimia 75 ya fedha
zinazokusanywa katika kodi na vyanzo vingine mbalimbali vya mapato katika
halmashauri hiyo huishia mifukoni mwa watendaji wa vijiji, kata na baadhi ya
watumishi wa serikali wenye wajibu wa kusimamia kazi hiyo.
Alitoa kauli
hiyo jana wilayani hapa, wakati akitoa hotuba ya ufunguzi ya mdahalo
ulioandaliwa na Mtandao wa Asasi zisizo za serikali wilaya ya Mbozi (MNN) na
kufanyika katika ukumbi wa Mkonongo.
Lengo la
mdahalo huo ni kuimarisha ushirikiano , uwajibikaji na uwazi kati ya
wabunge/madiwani , viongozi wa serikali na wananchi katika kufuatilia kero na
mahitaji ya huduma za jamii.
Dk. Kadeghe alisema kuwa baada ya kutembelea
katika vijiji mbalimbali wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali,
imebainika kuwa sehemu kubwa ya malalamiko ya wananchi yanahusu ufujwaji wa
fedha za umma.
Alisema
mbali na ubadhilifu huo alioubaini, lakini pia asilimia kubwa ya watendaji hao
wa vijiji na kata wamekuwa wakivunja sheria kwa kushindwa kusoma mapato na
matumizi, hali ambayo imesababisha wananchi wengi kujenga chuki na serikali.
Pia alisema
watendaji hao wamefikia hatua hiyo ya kufuja kiasi hicho kikubwa cha makusanyo
hayo kwa asilimia 75 bila kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na wengi wao
kushirikiana na baadhi ya wakuu wa vitengo katika Halmashauri hiyo.
Alisema
kutokana na hali hiyo ameamua kuingia vitani ili kupambana na wezi hao na kwa
kuanzia , atawashughulikia wale wote waliohusika katika ufisadi wa fedha zilizotengwa
katika miradi ya uchimbaji wa mabwawa.
Katika
kuhakikisha kuwa yuko tayari kupambana na vitendo hivyo vichafu ,Mkuu huyo wa
wilaya aliamua kutoa namba yake simu ya mkononi
0713-622750 kwa wananchi ili waweze kutoa taarifa wakati wowote pindi
wananchi wanapobaini kufanyika kwa vitendo hivyo.
Kwa upande
wake mtoa mada kutoka asasi ya Wadf-Mbozi, Happness Kwilabya, alishauri kuundwa
na kuanzishwa kwa chombo maalumu ambacho kitatoa nafasi kwa wapiga kura kukaa
pamoja na viongozi waliowachagua ili kujadili na kupeana mikakati ya kuendesha
jimbo lao, badala ya utaratibu wa sasa wa kutumia mikutano ya hadhara ambayo
wananchi hawapewi nafasi ya kujadiliana na mwakilishi wao.
Alisema hali
hiyo kwa muda mrefu imesababisha kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhusiano kati
ya makundi hayo na kusababisha kuendelea kudorora kwa michakato ya shughuli za maendeleo na
maendeleo kwa ujumla wilayani hapa.
Naye Neckwell
Kitta, kutoka asasi ya kujitolea ya masuala ya afya wilaya ya Mbozi (MBOHECO)
akieleza wajibu wa raia katika mchakato wa maendeleo, alisema ni lazima kila
mtu kufanya kazi kwa kujituma na
uaminifu mkubwa kwa kuwa kazi ndio huzaa
utajiri wa mali katika jamii na ndio chimbuko la ustawi wa jamii.
Aliongeza
kuwa kama kila mtu atajituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji mali
, kwa kutimiza nidhamu ya kazi anaweza kufikia malengo ya binafsi na yale ya
pamoja yanayotakiwa na kupangwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande
wa asasi za kiraia, alisema lengo kuu ni kuielimisha jamii kuhusu wajibu wa
kiraia,kisiasa na kisheria, pamoja na kuwezesha jamii na makundi
yaliyosahaulika kushiriki kikamilifu katika mchakato wa demokrasia na kufanya
maamuzi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment