Na. Lilian Lundo - MAELEZO
Katika
hotuba yake ya kwanza Mhe. Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe
Magufuli alipokuwa akifungua Rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alisema kwamba Serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika
ujenzi wa Viwanda.
“Viwanda
tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka
ndani, hususani kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na
maliasili nyingine,” alifafanua Rais Magufuli
Viwanda
hivyo vitatakiwa kuzalisha bidhaa ambazo zitatumiwa na watu wengi
nchini kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia ili kuwa na uhakika wa
soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje.
Licha
ya Serikali kuweka mkazo katika uanzishwaji wa viwanda nchini lakini
bado watanzania wamekuwa na fikra potofu juu ya bidhaa zinazotengenezwa
ndani ya nchi, wengi wao wanashusha thamani ya bidhaa hizo na kuziweka
katika kundi la bidhaa zisizo na ubora huku wakikimbilia bidhaa za nje
ya Tanzania.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipotembelea maonyesho ya
Viwanda yaliyofanyika kuanzia tarehe 07 hadi 11 Desemba 2016 alisema
kwamba Tanzania haitaweza kuwa Tanzania ya Viwanda ikiwa watanzania
wenyewe hawathamini bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.
Dkt.
Mpango alitoa mfano wa mashine zinazotengenezwa na SIDO ambazo zimekuwa
zikidharaulika kwamba hazina ubora wakati huo huo mashine hizo
zimetengenezwa kwa kuzingatia mazingira ya nchi yetu na gharama yake ni
ya chini ukilinganisha na zile zinazotengenezwa nje ya nchi.
“Haiwezekani
hata jembe la mkono liagizwe toka nje wakati kuna viwanda ndani ambavyo
vinauwezo wa kutengeneza majembe katika kiwango cha juu.” Alisema Dkt.
Mpango.
Ni
muda wa watanzania kubadilika na kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano
kwa kununua bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi ili kuipeleka nchi
kuwa na uchumi wa viwanda hatimaye kufikia uchumi wa kati.
Kamwe Tanzania haitaweza kufikia uchumi wa viwanda ikiwa sisi wenyewe tunakimbilia bidhaa zinazotoka nje ya Tanzania.
Ifike
hatua tuone bidhaa zetu ni bora zaidi kuliko bidhaa kutoka nje ya nchi.
Nchi nyingi zimeendelea kutokana na kuthamini bidhaa ambazo zimekuwa
zikitengenezwa ndani ya nchi.
Mfano
ni Nchi ya Japan, ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika uchumi wa
viwanda, mafanikio hayo yametokana na wajapani wenyewe kutokana na imani
ambayo wamejiwekea kwamba hakuna bidhaa inayotengenezwa Dunia yenye
ubora zaidi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini kwao.
Kwa
kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani kutaamsha morali kwa uanzishwaji
wa viwanda vingi hapa nchini, kwani watu wengi wamekuwa wakihofia
kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa hofu ya kukosa masoko ya bidhaa zao
na wengine wakihofia gharama ya uanzishwaji wa viwanda.
Ambapo
wengi wetu tumekuwa tukitafsiri kiwanda kama ni kuwa na mashine kubwa,
zenye gharama kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, na kusahau
kuwa kiwanda kinaweza kuundwa kwa kuwa na cherehani nne tu.
Hivyo basi, kwa kuwa na cherehani nne peke yake, tayari watu wanne wanakuwa wamepata ajira na kujikomboa kiuchumi.
Hivyo
uchumi huu wa viwanda ni fursa kubwa kwa vijana katika kutengeneza
ajira badala ya kusubiri ajira kutoka Serikalini au Mashirika Binafsi.
0 comments:
Post a Comment