Pages

Ads 468x60px

Saturday, October 21, 2017

Kenyatta aonya wanaotishia kuvuruga Uchaguzi Kenya


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewatahadharisha wanaotishia maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo pamoja na maandalizi ya uchaguzi mpya kwamba watakabiliwa vikali.
Aidha, ametoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi ambao umekumbwa na utata Alhamisi wiki ijayo 26 Oktoba.
Rais huyo amesema maafisa wa usalama wa kutosha wametumwa maeneo mbalimbali kuhakikisha kuna usalama siku hiyo.
“Tunapojiandaa kwa uchaguzi wa urais tareje 26 Oktoba, ni muhimu kudumisha amani, sawa na tulivyofanya (Agosti) na nyakati nyingine awali,” amesema.
“Kupiga kura kuwachagua viongozi tunaowataka ni haki ambayo ilipiganiwa na mababu zetu, na lazima tuilinde.”
“Sheria itatumika kwa njia sawa bila kujali hadhi yako katika jamii au siasa, hakuna atakayesazwa. Kwa wale wanaofana wakati wa vurugu, siku zenu zinafikia ukingoni, sheria itachukua mkondo wake na mtaadhibiwa ipasavyo.”
Kiongozi huyo alikuwa akihutubu wakati wa sherehe ya Siku ya Mashujaa ambayo huadhimishwa kila tarehe 20 Oktoba kuwakumbuka mashujaa waliopigania uhuru pamoja na Wakenya wengine waliotoa mchango wa kipekee kwa taifa baada ya uhuru.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alijiondoa kutoka kwenye uchaguzi huo wa Alhamisi na amesisitiza kwamba hakutakuwa na uchaguzi siku hiyo.
Badala yake amewahimiza wafuasi wake kuandaa maandamano kote nchini humo.
Kiongozi huyo wa upinzani ameongoza mkutano wa kisiasa eneo la Bondo, magharibi mwa Kenya ambapo amewahimiza Wakenya kuwa na umoja na kudumisha amani.
Bw Odinga amekuwa akishinikiza mageuzi yafanywe katika tume ya uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mpya.
Miongoni mwa mabadiliko hayo, alitaka afisa mkuu mtendaji Ezra Chiloba ang’atuke pamoja na maafisa wengine wakuu katika tume hiyo.
Taarifa zinasema Bw Chiloba ameamua kwenda likizo ya wiki tatu kuanzia Jumatatu, jambo ambalo litahakikisha kwamba hatakuwepo wakati wa kufanyika kwa uchaguzi.

0 comments:

Post a Comment